Madaktari 10 hatiani, waadhibiwa

Madaktari 10 hatiani, waadhibiwa

AFYA

Dar es Salaam.
Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), limewafungia leseni ya kutoa huduma madaktari sita, huku wanne wakipewa onyo kali baada ya kutiwa hatiani, kwa makosa ya ukiukwaji wa kanuni za maadili na utendaji wa kitaaluma. Ukiukwaji huo ulichangia madhara kwa wagonjwa, ikiwamo kupata ulemavu na vifo. Kwa kufungiwa kwao, hawatatoa huduma za afya mpaka adhabu zao zitakapokwisha, ikiwa tu haitaamriwa kufutiwa kabisa leseni.

Mwenyekiti wa MCT Profesa David Ngassapa alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kusikilizwa kwa mashauri tisa uliowagusa madaktari kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya, kati ya Januari 22 hadi 26, 2024. Anasema pande zote husika zilifahamishwa kuhusu haki ya kukata rufaa iwapo hawataridhika na uamuzi dhidi yao, kama inavyoainishwa katika kifungu cha 43(2), (3) na 44 cha sheria ya udaktari, udaktari wa meno na afya shirikishi.

Profesa Ngassapa aliwataja madaktari hao na vituo walikokuwa wakitolea huduma kwenye mabano kuwa ni Dk. Vindhya Pathirana (Kituo cha Afya Cradle cha Msasani, Dar es Salaam), Dk. Issa Nyangalaga (Kituo cha Afya Kibaoni, Ifakara – Mji, Morogoro), Dk. Aziz Mnkombe (Hospitali ya Wilaya Mkuranga, Pwani), Dk. Daniel Massawe (Hospitali ya Rufaa Mbeya), Dk. Getruda Mungale (Hospitali ya Wilaya Kigamboni, Dar es Salaam) na Dk. Mulindwa Mazana (Zahanati ya Kasulwa, Manispaa ya Kigoma Ujiji).

Profesa Ngassapa amesema Dk. Massawe amefungiwa leseni kwa miaka miwili na ameamriwa kuacha mara moja kufanya upasuaji wa kibingwa wa mifupa hata atakapomaliza kutumikia adhabu. Dk Massawe alikutwa na hatia kwa kutoa huduma ya upasuaji wa mifupa nje ya utaratibu wa taaluma yake, ambayo haimruhusu kufanya hivyo na kuwasababishia ulemavu wagonjwa. “Daktari huyu ameamriwa kugharimia matibabu ya wagonjwa Martha Mtega na Joseph Alphonce, ambao aliwasababishia ulemavu kutokana na upasuaji usioridhisha,” anasema Profesa Ngassapa. Pia Dk. Massawe atatakiwa kwenda mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja katika hospitali maalumu kwenye kitengo cha upasuaji, kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu kumalizika.

Dk Vindhya yeye amefungiwa kutoa huduma kwa miaka miwili, huku akielekezwa kwenda kwenye mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja katika hospitali ya kufundishia kwa mwaka mmoja kwa gharama zake, kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu. Msajili wa Baraza la Madaktari, Dk David Mnzava anasema Dk Vindhya, ametiwa hatiani kwa kumzidishia mgonjwa dawa aina ya Methotrexate licha ya kushauriwa. Pia alizuia mgonjwa kupatiwa rufaa kwa wakati alipozidiwa, hivyo kusababisha kifo chake.

Dk Nyangalaga yeye amefungiwa leseni kwa mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kuondoka kituoni wakati akiwa zamu bila kutoa taarifa na kusababisha kifo cha mjamzito ambaye aliukosa huduma. Dk Nyangalaga ameelekezwa kwenda mafunzo ya weledi, maadili ya kitaaluma na huduma kwa mteja kwa mwaka mmoja kwenye hospitali ya ngazi ya mkoa katika idara ya mama na mtoto, kwa gharama zake kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu.

Kwa upande wake Dk Mungale, Profesa Ngassapa amesema daktari huyo amefungiwa miezi sita baada ya kubainika kuwa akiwa zamu alishindwa kuwahudumia kikamilifu wagonjwa na kushindwa kuwapa rufaa. Ameelekezwa kwenda kwenye kliniki ya mafunzo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha wagonjwa wa dharura kwa gharama zake, na kufanyiwa uchunguzi wa afya kabla ya kurudishwa kutoa huduma baada ya muda wa kutumikia adhabu.

Mwingine aliyepewa adhabu za kufungiwa miezi sita ni Dk Mnkombe ambaye ametiwa hatiani kwa kushindwa kumhudumia mjamzito aliyehitaji huduma ya dharura, hivyo kuchangia kifo chake. Kwa upande wake Dk Mazana ameamriwa kuendelea kutumikia adhabu ya kufutiwa leseni baada ya maombi yake ya mapitio ya hukumu kutupiliwa mbali. Alipewa adhabu hiyo kwa kumfanyia upasuaji mkubwa mgonjwa katika zahanati, kinyume cha miongozo ya utoaji huduma na hivyo kumsababishia mgonjwa madhara makubwa.

Profesa Ngassapa amewataja madaktari waliopewa onyo kuwa ni Dk Living Colman wa Hospitali ya Saifee (Kinondoni, Dar es Salaam) ambaye alichelewa kumhudumia mjamzito aliyepata changamoto wakati wa kujifungua na kusababisha kupoteza damu nyingi na hatimaye kifo na Dk Rajah Chomboko wa Kituo cha Afya Kibaoni (Ifakara – Mji, Morogoro), ambaye ametiwa hatiani kwa kushindwa kumpa huduma stahiki mjamzito na kumpa rufaa kwa wakati, hivyo kusababisha kifo chake.

Kadhalika Luma Kigota ambaye ni mtaalamu wa tiba kwa vitendo (Kituo binafsi cha Kilulu, Temeke) alikutwa na hatia kwa kutoa huduma ya tiba kwa vitendo katika kituo kisichosajiliwa na bila kufuata miongozo stahiki kinyume na Kanuni za Maadili Kitaaluma zinazomtaka mtoa huduma kuzingatia utu na heshima kwa mgonjwa, huku Dk. Shafuri Ngaboli (Kituo cha afya Kabuku, Handeni mkoani Tanga) akitiwa hatiani kwa kushindwa kumhudumia mjamzito kutokana na kuwa nje ya kituo cha kazi huku akiwa zamu, pia kushindwa kumpa rufaa kwa wakati na kusababisha afariki dunia akiwa kituoni hapo.

Chanzo: Mwananchi

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...