Na Shani Nicolaus, Media Brains
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia miradi minne yenye thamani ya zaidi ya shillingi bilioni 7 ikiwemo mradi wa ujenzi kituo cha Afya cha Kinondoni ambao umeshindwa kukamilika kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 6, 2024 wakata akitoa taarifa ya utendaji kazi wa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2023 hadi Desemba 2023, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Ismail Seleman, amesema kuwa katika ujenzi wa kituo cha afya kinondoni wenye thamani ya Sh 1, 641, 561, 979.60 mkandarasi ameomba aongezewe muda ili aweze kukamilisha.
“Ufuatiliaji wa karibu unaendelea kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa ubora na kuzingatia thamani ya fedha,” amesema Seleman.
Ameongeza kuwa wamepokea malalamiko 51 yaliyohusu rushwa ambapo yanaendelea kushughulikiwa katika hatua mbalimbali ili yapatiwe ufumbuzi.
Amesema kuwa malalamiko hayo yalikuwa yanahusu tuhuma zilizopo katika sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa (PCCA) pamoja na sheria nyengine (OL).
“Tuhuma zote zinafanyiwa uchunguzi wa awali kabla ya kutoa ushauri kwa walalamikaji, ni muhimu kufanya uchunguzi wa awali kabla ya kutoa ushauri kwa walalamikaji,” amesema Seleman.
Akizungumzia utekelezaji wa programu ya Takukuru Rafikim, amesema wamezifikia kata nne kupitia vikao na wadau na kufanikiwa kuzipatia ufumbuzi wa kero mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari, kufanya semina 26, uimalishaji wa klabu za wapinga rushwa sita.
“Tunatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Takukuru na kuwasihi wapatapo taarifa za rushwa watoe taarifa kupitia mitandao yote ya simu kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kupitia namba ya dharula 113, Kuzuia rushwa ni Jukumu lako na Langu; Tutimize wajibu Wetu,” amesema Seleman.