SERIKALI imekiri kuwepo kwa ujenzi holela katika maeneo mbalimbali licha ya uwepo sheria zinazoweka masharti ya ujenzi katika miji nchini, huku ikisema chanzo kikubwa ni ukuaji wa kasi miji midogo kutoka vijiji unaotokana na shughuli za kibinadamu.
Hata hivyo Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda ameliambia Bunge mjini Dodoma kuwa, kutokana na hali hiyo wizara yake imekuja na mikakati ya kupima nchi nzima hadi vijijini.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Asia Sharif Omar, Pinda amesema kampeni ya kupima vijiji inayofanywa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi sambamba na upimaji miji unaofanywa na halmashauri kwa ushirikiano na wizara, ni sehemu ya juhudi za kupambana na ujenzi holela.
Kadhalika Pinda amesema ipo miradi ya urasimishaji wa makazi na upimaji shirikishi ambayo pia ni sehemu ya mikakati ya kupamabana na ujenzi holela na kuweka wazi kuwa Serikali itaendelea kukabiliana na changamoto za ujenzi wa aina yoyote usiozingatia taratibu na sheria za nchi.
Katika hatua nyingine Pinda amezielekeza mamlaka za miji na wilaya kote nchini kuhakikisha maendelezo yoyote yanayofanywa yanazingatia na kufuata mipango kabambe ya maeneo husika.
Kwa mujibu wa Pinda, kunakosekana usimamizi wa mipango iliyowekwa na mamlaka hizo, licha ya kwamba baadhi ya meneo hasa majiji makubwa tayari yana mipango mahususi (mpango kabambe) ya kuendelezwa kwake.
“Nitoe rai kwa mamlaka za miji na majiji kuzingatia yaliyopitishwa na mamlaka zao kwa kuhakikisha miji inatoka na sura nzuri kwa kuzingatia mipango kabambe na hili la Mwanza wazingatie kile walichokubaliana,’’amesema Pinda bungeni Februari 6, 2024.
Naibu Waziri huyo alikuwa aikijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nyamagana mkoani Mwanza, Stanslaus Mabula aliyetaka kujua mikakati ya serikali kuhakikisha maendeleo yanayofanyika kwenye halmashauri hayavunji au utekelezaji wake hauendi kinyume na mpango kabambe kwa kufanyiwa matumizi mengine yasiyokusudiwa.
Mhe. Pinda alitoa amesema Jiji la Mwanza linapaswa kuzingatia kile walichokubalina kwenye mpango kabambe kwa kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimetumika wakati wa kuandaa mpango huo wa uendelezaji wake.