Mlima unaomsubiri Nchimbi kiti cha Katibu Mkuu CCM

UTEUZI wa Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaweza kufananishwa na samaki aliyerudishwa majini kwani alianza kuhudumu ndani ya chama hicho tangu akiwa kinda, alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana (UVCCM) mwaka1999 akiwa na umri wa miaka 27.

Katika uteuzi huo ulioidhinishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Januari 15, 2024, unafungua ukurasa mpya wa harakati za kisiasa katika nchi, hasa kutokana na kuwako kwa chaguzi kuu mbili nchini. Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.

Kwa mujibu wa taratibu za CCM, Katibu Mkuu ndiye msimamizi wa uchaguzi katika mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea kupitia chama hicho.

Kwa uteuzi huu unaotokana na NEC iliyoketi Visiwani Zanzibar, Balozi Dk. Nchimbi anakuwa katibu mkuu wa CCM wa 12 wakijumhishwa Makatibu Wakuu Watendaji wawili, Pius Msekwa na Daudi Mwakawago. Anaingia ofisini wakati nchi tayari ina joto kubwa la kisiasa kuhusu katiba mpya, mabadiliko ya sheria za uchaguzi, tume ya uchaguzi na suala la wagombea katika nafasi mbalimbambali ndani na nje ya chama chake.

Katibu huyo mpya pia anaingia kibaruani huku mitandao ya kijamii ikiwa imesheheni taarifa za udadisi iwapo mwakani CCM itampa au la nafasi ya kugombea urais Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM. Rais Samia alirithi kiti cha urais kutoka kwa Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 40 (4) inatoa fursa kwa Rais Samia kuwania kipindi cha pili kwa kuwa alichorithi kutoka kwa Rais Magufuli atahudumu kwa zaidi ya miaka mitatu ambacho kitahesabika kuwa ni kipindi chake cha kwanza, hivyo kuwa na shufaa ya awamu ya pili.

Kadhalika Dk. Nchimbi anakabidhiwa kiti cha katibu mkuu wakati ambao mabadiliko ya nafasi za uteuzi yamekuwa ni ya kasi sana, kote ndani ya chama hicho na hata serikalini ambako uteuaji na utenguaji umeshika kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Pia, Katibu huyo mpya anaingia ofisini wakati ambao kumekuwa na hali ya uchumi isiyotabirika duniani na nchini, huku bidhaa wa vyakula na nishati vikipanda bei kwa kasi kubwa. Hali hii ya uchumi kuwa mgumu imeibua mijadala na hoja ya kutaka serikali ichukue hatua mahususi za kubana matumizi ili kuleta nafuu kwa wananchi.

Dk. Nchimbi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Daniel Chongolo ambaye aliandika barua ya kujiuzulu Novemba 27, 2023 kwa Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Sababu za kujiuzulu kwa Chongolo

Chongolo amemaliza muhula wake kama Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuandika barua ya kujiuzulu na kuhitimisha takribani miaka miwili na miezi saba ya kutumikia nafasi hiyo.

Kulingana na barua hiyo ya Chongolo, sababu alizozitaja kuachia wadhifa huo ilikuwa ni pamoja na yeye kuchafuliwa katika mitandao ya kijamii huku msingi mkuu wa barua hiyo ukiwa ni kuwajibika kama kiongozi kwa maslahi ya chama hicho kilichoko madarakani.

Chongolo aliandika barua hiyo baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa siku 942 tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo wa juu wa CCM Aprili 30, 2021.

Kuteuliwa kwa Dk. Nchimbi ni hitimisho la minong’ono ya muda mrefu kutoka kwa wadadisi wa siasa wa Tanzania ambao waliokuwa wakihusisha jina la mwandiplomasia huyo kurithi kiti hicho cha Chongolo pamoja na majina mengine mawili ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela na Mbunge wa Ismani, William Lukuvi.

Dk. Nchimbi ni nani?

Dk. Nchimbi ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa 11 wa CCM, alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya. Elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 – 1986.

Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara.

Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Dk. Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Dk. Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

Alisoma shahada ya uzamili ya usimamiz wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).

Dk. Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003–2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Dk. Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM.

Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu.

Dk. Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini.

Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.

Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dk Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.

Rais Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013 kwa shinikizo, baada ya ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli juu ya “Oparesheni Tokomeza”.

Kuna nyakati Dk. Nchimbi amekuwa kiongozi asiyeweza kutoa majibu kwa maswali magumu juu ya matukio ya hatari, ya kikatili na kuhuzunisha yaliyotokea wakati yeye ndiye mwenye dhamana.

Alipokuwa na dhamana ya ulinzi wa ndani wa nchi kuna matukio mengi makubwa yalijitokeza na hadi leo hakuwahi kuyatolea ufafanuzi na majibu ya kutosha.

Moja ni tukio la utekaji na uteswaji wa Dk. Stephen Ulimboka lililotokea usiku wa Juni 26, 2012. Kuuawa kwa Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, tena akiwa kazini na mikononi mwa vyombo vya Dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa.

Baada ya kifo cha Mwangosi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa ambaye aliingilia majukumu ya kamanda wa polisi wa wilaya kwa kuvamia eneo ambalo Chadema walikuwa wakifungua matawi na kuwa kichocheo cha amri iliyosababisha kuuawa kwa Mwangosi, alipandishwa cheo. Haya yalitokea chini ya uongozi wa Dk. Nchimbi.

Pili, ni kupigwa risasi na kuuawa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko, Kigoma Januari 2013, katika mazingira ya kutatanisha. Dk Nchimbi akiwa waziri na hadi alipoondoka, tukio hili limebakia tu hewani.

Tatu, tukio la Mwandishi wa Gazeti la Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa “kimakosa polisi walidhani Matutu ni jambazi”. Pamoja na uzembe huo wa polisi, hakuna hatua zilizochukuliwa.

Nne, siku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013, Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda akiwa getini akijiandaa kuingia nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, alivamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana. Katika uhalifu huo Kibanda alipoteza jicho, kuvunjwa mifupa kuzunguka taya, kukatwa kidole na kuumizwa sehemu mbalimbali za uso.

Balozi Nchimbi aliteuliwa na Rais wa awamu ya tano hayati Dk. John Magufuli kuwa balozi wa Brazili Desemba 3, 2016, kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan hajamhamishia kuhudumu nafasi hiyo nchini Misri.

Baadaye Rais Samia alimrudisha nyumbani baada ya kumaliza muda wake na sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM.

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...