Vita ya Israel vs Hamas yafichua makengeza ya vyombo vya habari

MIAKA kadhaa iliyopita bila kutarajia nilijikuta katika mabishano na Mwalimu wangu huko ughaibuni tukiwa darasani. Ubishi huu uliibuka wakati huo kituo cha Al Jazeera kikiwa bado ni kichanga sana. Alikuwa ametushawishi tuwe tunaangalia habari za kituo hicho mbali tu ya kuangalia BBC na CNN ambazo kwa kweli ndivyo vilikuwa, na bado ni, vyombo vikubwa vya habari vya nchi za magharibi.

Moshi na moto vikifuka baada ya wanajeshi wa Israel kugonga mnara wa juu katika mji wa Gaza. Picha – [Ashraf Amra/Reuters]

Nilimwambia Mwalimu wangu wakati ule kwamba, kinachoonyeshwa na Al Jazeera ni kinyume cha kile kinachoonyeshwa na BBC na CNN, kwa sababu vyombo hivyo ukiwa na jicho la kidadisi sana utagundua tu kwamba vinaegemea upande mmoja katika ripoti zao.

Kumbukumbu hii ilinirejea Jumamosi iliyopita, Oktoba 7. 2023 wakati ninafuatilia jinsi vyombo vya habari vinaripoti yanayoendelea Mashariki ya Kati katika vita mbaya kuliko zote ambazo zimepata kutokea katika karne hii ya 21 kati ya kikundi cha Hamas dhidi ya taifa la Israel.

Niseme wazi kabisa, kwamba siungi mkono umwagaji wa damu wa binadamu yeyote. Siungi mkono unyanyasaji wa kikundi au mtu dhidi ya mwingine, na vivyo hivyo siungi mkono mwenye nguvu kujiona ana uwezo na haki ya kumburuza mnyonge atakavyo. Kwa maana hiyo, mzozo wa Mashariki ya Kati baina ya Taifa la Israel na Palestina ni kielelezo kingine cha jumuiya ya kimataifa kukosa uhalali katika kushughulikia mizozo kwani suala hili limekuwa sugu kwa miongo karibia minane sasa tangu kutambuliwa kwa taifa la Israel mwaka 1948. Jamii ya kimataifa imefunikwa na undumilakuwili mkubwa!

Sasa nirejee katika hoja ya ubishi kati yangu na Mwalimu wangu zaidi ya miongo miwili iliyopita. Kwamba ni kwa jinsi gani vyombo vya habari vinavyoripoti matukio mbalimbali duniani vinajikita katika maadili ya uandishi wa habari? Je, kuna kuzingatia weledi kwa maana ya kutokuegemea upande wowote? Je, kuna uzingatiaji wa miiko ya uandishi kama vile kutokuonyesha picha za watoto, maiti, watu wenye majeraha makubwa na picha zinazoogofya kwa ujumla wake katika uwanja wa vita? Je, kuna haki na usawa?

Katika tathmini yangu, nimejikuta ninajiuliza maswali, kwamba ni kwa nini kwa mfano Al Jazeera wanakuwa wepesi na rahisi kwao kupata taarifa za matukio ya upande wa Hamas/Palestina, kama ambavyo wamekuwa wakihoji walioathiriwa na mashambulizi ya Israel katika ukanda wa Gaza, na pia wamekuwa wakionekana kupata ushirikiano wa karibu zaidi na upande wa Palestina? Kwa upande wa pili, tathmini yangu inaonyesha kwamba ni kwa nini CNN na BBC wanayapata kwa karibu, kiurahisi na kwa undani zaidi matukio ya madhara ya mzozo huu mbaya kwa upande wa Israel kwa kina zaidi kuliko wenzao wa Al Jazeera? Kwa mfano, BBC na CNN wameonekana wakiwa huru zaidi katika mitaa mbalimbali ya miji ya Israel, wakipita karibu kabisa na wanajeshi wanaowasaka wafuasi wa Hamas ambao wanaelezwa kujipenyeza katika miji hiyo na kufanya mauaji ya kufuru kubwa?

Lakini tathmini yangu haikuishia hapo tu, nimetafakari hata aina za picha za video katika matukio haya ambazo zinasambazwa na vyombo hivi vikubwa vya habari duniani, usipoangalia kwa jicho la ziada, hutaelewa kwamba kila kimoja kina ajenda.

CNN na BBC wanabeba ajenda ya Israel, wanaonyesha kwa kina zaidi madhara ambayo yamesababishwa na Hamas, wanaonyesha jinsi Hamas walivyokosa utu kiasi cha kusababisha mauaji ya watoto, wanawake na wazee. Kwa upande mwingine Al Jazeera nao wanafanya hivyo hivyo. Wanaonyesha kwa kina jinsi mji wa Gaza umebomolewa, majengo ya ghorofa yanaporomoshwa hadi chini.

Yanakuwa kifusi kitupu. Wanaonyesha majeruhi, hali ya huduma ya hospitali, wanaonyesha na kufanya mahojiano na ndugu na jamaa wa Wapalestina waliouawa na majeshi ya Israel. Kwa kufupi ni kwamba ingawa kuna chembechembe za kujaribu kuonyesha na upande wa pili wa vita hivi baina ya vituo hivi vitatu, bado mizania ya habari hizi hazionyeshi kuwa waandishi na vituo vyao hawaegemei upande mmoja wa mzozo huu.

Hali ilinisukuma hadi kukumbuka jinsi vita ya Iraq ya mwaka 2003 ilivyoripotiwa na vyombo hivi. Mizania haikuwa sawa mwaka 2003 na hata leo miaka 20 baadaye, mizania imezidi kuwa ile ile licha ya mitandao ya kijamii kutoa changamoto kubwa kwa vyombo vya habari hasa kupitia citizen journalism.

Hakuna ubishi kwamba Israel ni mshirika wa nchi magharibi kama vile Marekani na Uingereza.  Mataifa hayo pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Italia wamekwisha kutoa tamko lao juu ya mzozo wa sasa, na wamewalaani Hamas vilivyo. Katika sura hii, ingawa Hamas siyo wawakishi halali wa Wapalestina hasa katika mapambano yao ya kudai ardhi yao na kutambuliwa kwa taifa lao na kuachwa lijitawale lenyewe na kuondoka chini ya ukandamizi wa Israel, ni vigumu kuwatenganisha na mapambano ya kutaka kujitawala kwa taifa la Wapalestina.

Katika sura hii ya vyombo vya habari vikubwa vya magharibi na ukitafakari misimamo ya mataifa hayo juu ya mzozo wa Israel na Palestina, haiyumkiniki kuona vyombo hivi vikitoa fursa sawa kwa pande zinazozozana katika mgogoro huu mkongwe zaidi wa Mashariki ya Kati.

Ni katika tathmini hii ninajikuta nikijiuliza hivi habari ni nini? Nani anaamua nini kirushwe hewani na kwa mwonekano upi? Na huo muonekano unabeba ajenda ipi na ni ya nani? Maswali haya yananifanya nijiulize kwa mfano, katika dunia ya sasa ambayo mitandao ya kijamii imefanya mfumo na njia ya kupata taarifa na habari mbalimbali kuwa rahisi zaidi kwa sababu ya maendeleo ya tekiolojia ya kidijitali, vyombo rasmi vya habari na waandishi wanaweza vipi kuonekana wakweli na watu wanaotimiza wajibu wao bila kuegemea upande wowote? Bado wataendelea kuaminiwa na jamii?

Kwa mfano, ndani ya mitandao ya kijamii kama X, WhatsApp, Meta, Instagram na mingine mingi, zipo taarifa na habari ambazo vyombo vikuu vya habari vinavyofuatilia vita hivi vinazipiga mgongo, hasa inapokuwa hazinufaishi au kuonyesha kubeba upande wao katika kusukuma ajenda ya upande unaopendelewa katika kadhia ya sasa ya Mashariki ya Kati.

Pengine kwa wasomi na wanazuoni wanaofundisha masomo ya uandishi wa habari, ni wakati sasa wa kujiuliza hivi kweli maadili tunayowalisha wanafunzi wa masomo ya uandishi wa habari yanazingatiwa? Je, vyombo vya habari vikubwa vya dunia kwa mwenendo wao juu ya mgogoro wa Israel na Hamas/Palestina vinaandika na kutangaza ukweli na ukweli mtupu? vinaandika na kutangaza habari sahihi, vinazingatia haki na usawa kwa pande zote mbili za mzozo huu, vinaepuka kuegemea upande mmoja? Nimejiuliza haya maswali machache ambayo yamejikita katika msingi mikuu ya maadili ya uandishi wa habari. Najiuliza tena na tena, je, vyombo vya habari vinaupa ulimwenmgu ukweli mtupu kuhusu vita ya Israel na Hamas/Wapalestina?  

spot_img

Latest articles

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

TANZANIA KUPAMBANA NA JANGWA

Na Mwandishi wetu Serikali imejipambanua katika kupambana na kuenea kwa jangwa, kurejesha ardhi iliyoharibiwa pamoja...

More like this

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...