Rwanda mbaya ya 1995, leo inatuduwaza

KATIKA pitiapitia yangu kwenye mitandao ya kijamii nilikutana na ujumbe ufuatao:

Nakumbuka kuona kwenye TV tangazo …kwenye kampeni za uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi (1995) likionyesha picha za mauaji ya Rwanda na kuonya wapiga kura kuwa wakichagua upinzani, yatawafika ya Rwanda. Leo miaka 30 baadaye, ukijaribu kuisifu Rwanda kwa mafanikio yoyote, wanasiasa walewale watakutaka usitumie mfano wa Rwanda maana Rwanda ni sawa na kiji-mkoa tu!”

Jiji la Kigali, Rwanda-Picha na Mtandao.

Nimeguswa na simulizi hii hasa tunapokabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi nchini kwa sasa. Kikubwa ni mgawo wa umeme. Hakuna ubishi kwamba Rwanda ni nchi ndogo ikilinganishwa na Tanzania kwa maana ya ukubwa. Tanzania ina km za mrada 945,087 wakati Rwanda ni 26,338km2 ikizidiwa ukubwa na mikoa 15 ambayo ni Tabora (76,151km2), Moro (70,799km2), Rukwa (68,635km2), Lindi (67,000km2), Ruvuma (63,498km2), Singida (49,341km2), Manyara (46,359km2), Dodoma (41,311km2), Arusha (37,576km2), Kigoma (37,037km2), Mbeya (35,954km2), Pwani (32,407km2), Kagera 28,388km2), Songwe (27,656km2) na Tanga (26,808 km2).

Hata hivyo, ni vigumu mtu kuipuuza Rwanda kwa maana ya ilikokuwa mwaka 1994 wakati mauaji kimbari yaliyogharimu uhai wa watu takriabani 800,000 ikiwa imeparaganyika kabisa na kuwa vipande vipande. Huku raia wake wakiishi kwa kutegemea misaada zaidi. Katika madhila hayo, zaidi ya raia wake 2,000,000 walikuwa wameikimbia nchi yao kwenda kuishi kama wakimbizi. Tanzania ilikuwa imehifadhi takriabni wakimbizi 800,000 katika kambi ya Benaco iliyokuwa Ngara, Kagera. Hii wakati huo ilitajwa kuwa ni kambi kubwa ya wakimbizi kuliko zote duniani. 

Ni hakika tukiitazama Rwanda, ingawa haina rasilimali zozote za maana ikilinganishwa na Tanzania, huwezi kuipuuza kwa maana ya kujijenga upya kutoka nchi iliyoparaganyika mwaka 1994 mpaka sasa inaweza kuvutia wawekezaji.

Watu wengi waliopata fursa ya kufika Rwanda wana simulizi nyingi juu ya mambo mengi. Kikubwa wanataja jinsi jiji la Kigali lilivyo safi, limepangwa na nidhamu ya uendeshaji magari barabarani ni ya hali ya juu sana. Kwamba bodaboda ambazo zimetushinda kabisa jinsi ya kuzidhibiti hapa nchini, zikivunja sheria mbele ya trafiki- kutozingatia taa za kuongoza vyombo vya moto kwenye makutano ya barabara, kutokuvaa kofia ngumu, kupakia abiria zaidi ya mmoja (mshikaki), kupita upande wa barabara usioruhusiwa na kila aina ya vurugu, ndani ya Rwanda vitu hivyo haviwezekaniki kabisa kutokea. Nidhamu ni kubwa mno. Hizi si simulizi tu, binafsi nilipata kushuhudia haya.

Nimetaja vitu vidogo sana hapa ili kupima utayari wetu wa kuwajibika, kujituma na kufanya vitu katika mpangilio unaoeleweka. Kwamba Rwanda inayoingia takribani mara 36 ndani ya Tanzania, ni hoja ya msingi ya kuepuka kuyafananisha mataifa hayo mawili.

Kwamba hata ukitazama pato la ndani mataifa hayo, Tanzania Dola bilioni 75.7 hivi wakati Rwanda ni Dola bilioni 13.3, nchi hizo zikiwa na pato la raia wake la Dola 1,146 kwa Tanzania na Dola 821 kwa Rwanda, takwimu hizo bado zinaonyesha tofauti kubwa iliyoko baina ya nchi hizo. Kwamba ungeamua kuhamisha barabara zote za Tanzania na kuzibandika ndani ya Rwanda, nchi nzima ingefunikwa kwa lami hadi kusiwe na hata eneo la ardhi la kupanda hata mche wa mchicha, bado kipo cha kujifunza kutoka Rwanda.

Kama alivyochokoza mada msemaji wa kwenye mitandao hapo juu, kwamba kuna la kuisifu Rwanda leo, kama vile ambavyo ilikuwa mfano mbaya mwaka 1995 karibia miaka 30 iliyopita, nchi hiyo imejikwamua kutoka katika mashaka makubwa. Imepiga hatua. Tunaona wawekezaji kutoka ughaibuni wakimiminika Rwanda kuwekeza, ijapokuwa haina rasilimali za maana. Tumeona ikitajwa kuwa na uchumi unaokuwa vema, tumesikia na kuona ikiwa simulizi ya mafanikio katika ukanda wetu, hata kama demokrasia yake ina walakini mkubwa. Je, nini kimeifanikisha Rwanda kwa kiwango hicho?  Hii inaweza kuwa mada ya mjadala wa siku nyingine.

Tujiulize tu, kama nchi ndogo kama Rwanda ambayo ilifikia hatua ya kukaribia kabisa kutoweka kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, leo imefika hapo kwa juhudi za jasho na damu, je, sisi ambao tuliwahifadhi wakiwa wakimbizi, tukisaidia hata mazungumzo ya kurejesha amani nchini kwao, ni kwa nini kasi yetu ya maendeleo haifanani na ukubwa wetu, rasilimali zetu, uwezo wa watu wetu, wingi wa watu wetu, na kila kitu kikubwa kikubwa tulichojaliwa na muumba?

Taifa kwa sasa liko kwenye ratiba kali ya mgawo wa umeme, ingawa wazalisha umeme wanazuga eti kuna ratiba ya upatikanaji wa umeme. Ni sawa tuna na kusema bilauri imejaa maji nusu au bilauri iko tupu nusu. Jambo ni lilelile. Sasa katika nchi kama Tanzania ambayo tumebarikiwa kuwa na gesi asilia, ambayo tayari imeshachimbwa na miundombinu yake ya kuisafirisha kujengwa hadi kwenye mitambo ya kuzalisha umeme, ni kitu gani kimekwaza mipango ya kuhakikisha uzalishaji wa umeme wa uhakika kwa chanzo cha gesi asilia? Kwa nini tumeshindwa kutumia rasilimali gesi asilia kuwa na uhakika wa umeme hivyo kutuepusha na fadhaa hii ya mgawao wa umeme? 

Kwa nini tusijulize maswali magumu kama taifa kwamba kama tumeshindwa kudhibiti bodaboda barabarani kwa trafiki kusalimu amri, au kama tumeshindwa hata kupanga wachuuzi kwenye mitaa ya miji yetu, au kama tumeshindwa hata kuzoa taka katika miji yetu huku tukiacha mitaro ya maji machafu kuwa dampo za muda, hivi tunaweza kufanya nini basi?

Ni hakika hakuna hata kipande cha nusu inchi ya nchi hii ambacho hakina msimamizi. Tuna wenyeviti wa serikali za mitaa, tuna watendaji wa mitaa, tuna madiwani na mabaraza yao, tuna wabunge na bunge lao, tuna serikali kuu na vyombo vyake vyote- baraza la mawaziri, polisi, jeshi, mahakama, usalama wa taifa kuna mpaka mgambo, lakini bado tumekwama. Tena tumekwama sana.

Serikali inatumia mabilioni ya fedha kujenga barabara za kiasasa katika miji yetu. Mfano mzuri ni katika jiji la Dar es Salaam, lakini ukipita katika barabara hizo, maeneo karibu yote ya watembea kwa miguu yamegeuzwa kuwa vibanda vya wamachinga na masoko bubu ya kuuza bidhaa, miji imefurika kila aina ya takataka kutokana na biashara hizo ambazo ni kama imeshindikana kuratibiwa na kudhibitiwa.

Hakika tunapaswa kujihoji kama taifa kwamba ni nini hasa kimetukwamisha. Tuna kila kitu, kwa maana ya rasilimali, lakini tumekwama sana. Kama Rwanda ilikuwa mfano mbaya mwaka 1995 leo tuitumie kama mfano mwema huku tukijiuliza kama kaka mkubwa, tumedumazwa na kuduwazwa na nini?

spot_img

Latest articles

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...

TANZANIA YAWEKA REKODI MKUTANO WA WAHASIBU WAKUU AFRIKA

Na Mwandishi Wetu Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali...

More like this

Hivi vikosi kazi vimerejea kwa mlango wa nyuma?

KUNA kila dalili kwamba taifa letu kidogokidogo linakumbwa na hali ya kutokuaminiana. Hali hii...

Chondechonde Polisi msisababishe wananchi wakate tamaa

ALHAMISI iliyopita yaani Desemba 5, mwaka huu wa 2024 lilitokea tukio baya la kuhuzunisha...

Ufaransa yaipatia Tanzania Sh bilioni 323.4

Na Mwandishi Wetu Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo La Ufaransa (AFD) wamesaini mikataba...