‘Hali ilikuwa mbaya TANU ilipokuwa CCM’

Na Jesse Kwayu, Media Brains

KAMA kuna watu walifanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere kwa karibu sana na kwa muda mrefu zaidi katika utumishi wake wa umma, hakika hawezi kuwako anayemzidi mwanamke wa Kiingereza Joan Wicken. Huyu alikuwa ni katibu wake na mwandishi wa hotuba zake tangu Mwalimu ananza madaraka ya juu kabisa katika taifa hili.

Joan Wicken(kulia) akiwa na Malkia Elizabeth wa Uingereza na Hayati Rais Julias Nyerere. Picha| Tanzanian Affairs.

Wapo wanaomzungumzia Mwanamama huyu kama katibu (personal assistant) wa Mwalimu, mwandishi wa hotuba zake, mwandani wake (confidant), ubao wa kujisilizia (a sounding board) na zaidi rafiki. Wicken ni msaidizi pekee ambaye aliingia ofisini pamoja na Mwalimu mwaka 1961 na akafanya naye kazi mpaka alipostaafu urais mwaka 1985. Mwanamama huyo alifariki dunia mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 79 nchini kwao Uingereza.

Mengi ambayo alifanya akiwa na Mwalimu yanajulikana. Kikubwa kabisa ambacho Mwanamama huyo wa Kiingereza alifanyia taifa hili ni kuchanja mbuga katika Tanganyika yote miaka ya 1960 na 1961 akikusanya pesa (michango) ya wananchi, hasa wanachama wa TANU, kwa ajili kujenga chuo cha Kivukoni. Katika kitabu cha Joan Wicken kilichoandikwa na Aili Mari Tripp kilichochapishwa mwaka huu, kinaelezea maisha ya Mwanamama huyo na safari yake ya utumishi hapa nchini akiwa na Mwalimu Nyerere. Mwandishi anagusia vitu vingi ambavyo Wicken alisimulia katika mahojiano naye.

Joan Wicken, katika utumishi wa Mwalimu Julias Nyerere Tanzania, tangu akiwa mwanamke kijana hadi bibi kizee. Picha| Mtandao.

Hata hivyo, ukisoma kitabu hicho utagundua kuwa Wicken hakuwa tu mwandishi wa hotuba wa Mwalimu, bali alikuwa na kitu cha ziada sana katika utumishi wake. Anapozungumzia safari yake ya kuchanja mbuga kusaka pesa ya kujenga chuo cha Kivukoni, anaacha msisimko mkubwa sana wa nguvu iliyokuwa imejaa kwa wanachama wa TANU.

Utayari wa wanachama wa TANU wa kutoa na kujitoa kwa chochote katika zama hizo, wengi wakiwa hata hawajui kusoma na kuandika, lakini kwa hamasa ya chama chao waliona umuhimu na ulazima wa kuchanga chochote ili kujenga chuo. Ili kupiga hatua ya kujikomboa na kuwa huru.

Mwanamama huyo ambaye pia hata baada ya Mwalimu kustaafu bado alikwenda kufanya naye kazi chini ya Tume ya South South, anagusa mzizi mkuu wa matatizo ya taifa letu leo. Anagusa kiini cha tatizo linalotukabili leo kama taifa. Anasema kwa undani kabisa, alianza kuona TANU kidogo kidogo ikivalishwa rushwa. Na si mwingine aliyeanza kuvalisha chama hicho rushwa isipokuwa viongozi.

Anasema alianza kuona nguvu kubwa ya wanachama wake waliokuwa na hamasa kubwa ya kujenga taifa lao, wakiwa na uwezo wa kuwawajibisha viongozi, wakiwa na moyo wa kujitoa na kujitolea, ikianza kumezwa kidogo kidogo na viongozi. Kwamba ule uhuru wa kidemokrasia wa wanachama ukaanza kugeuka na kuanza kuonekana viongozi wakiwa juu na kuwa na nguvu kuliko wanachama.

Simulizi ya Wecken inaamsha maswali magumu sana juu ya chimbuko la rushwa ambayo kwa miaka na miaka imeota mizizi katika taifa letu. Kwamba kile chama cha TANU kilichozaa

CCM mwaka 1977 kilibadilika vipi kufikia kiwango cha chaguzi za chama hicho kuwa gulio kubwa la rushwa kila baada ya miaka mitano? Iwe ni miaka mitano ya kutafuta uiongozi ndani ya chama kuanzia ngazi ya tawi, kata, wilaya, mkoa hata taifa au hata katika nafasi za kuongoza dola? Kwa wanaokumbuka, mwaka 1995 baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi ulianza utaratibu wa kura za maoni ndani ya vyama, kwa kweli hasa ndani ya CCM, ili kumpata mgombea anayekubalika na wengi kugombea nafasi za kuchaguliwa katika madaraka ya dola- udiwani, ubunge na urais.

Joan Wicken. Picha:| Mtandao.

Utaratibu huu ambao ulipaswa kushamirisha na kukomaza demokrasia, ulikuja na makandokando yake. Kwamba ili mtu apitishwe kugombea nafasi hizo, ni lazima awe na pesa, na pesa hizo zitagawanywa kwa wale wanachama wanaoitwa wajumbe. Bila pesa huwezi kupata kura hizi.

Huu umekuwa ni utamaduni. Kwamba viongozi wanaoutaka uongozi ndiyo wananunua wanachama. Gulio la kura! Kwa kufanya hivyo wanachama wanakuwa wameuza kabisa nguvu yao kwa viongozi na uwezo wa kuwadhibiti. Katika kitabu cha Tripp anamnukuu Wecken akisema aliona mabadilio na hali kuwa mbaya sana juu ya rushwa hii ya madaraka, baada ya TANU kuwa CCM. Haya anayatamka kwenye ukurasa wa 144 wa kitabu hicho ambacho kipo kwenye maduka ya vitabu hapa nchini kwa sasa.

Mwanamama huyu siyo tu kwamba aliishi Tanganyika na baadaye Tanzania na kufahamu vema watu wake na mienendo yao, bali pia alikuwa karibu kabisa na kitovu cha madaraka makuuu ya nchi, Rais. Alisikia, aliona na kupata fursa ya kufahamu changamoto za kiuongozi ambazo viongozi wa wakati huo, mwaka 1961 hadi 1985 walipitia. Anaizungumzia rushwa katika staili ambayo anaamini wapaliliaji wakuu wa kansa hiyo ni viongozi. Kwamba baada ya kuanza kidogo kidogo kuiteka TANU ambayo nayo ilipogeuka na kuwa CCM, basi mambo yalikuwa mabaya zaidi.

Inawezekana tukadhani kuwa raia huyu wa Kiingereza alizusha kuhusu hali ya rushwa katika nchi yetu. Inawezekana pia kumpuuza kwamba alikuwa ametekwa na siasa za Ikulu ambako alitumika kwa miongo miwili na nusu mfululizo. Lakini, pia inawezekana tukampuuza kwa sababu kiwango cha rushwa katika jamii yetu kimekuwa ni kikubwa mno kiasi cha kugeuka kuwa utamaduni na mfumo rasmi wa maisha.

Kwa mfano, nani asiyejua kwamba shughuli ya kutafuta kura imekuwa ni kazi ya kudumu katika nchi hii? Yaani unafanyika uchaguzi mwaka huu washindi wanapatikana, wanaapishwa na kuanga uongozi katika ngazi yoyote waliopata, na hapo hapo wanaanza tena harakati za kutafuta kura kwa ajili ya uchaguzi unaofuata. Yaani mfumo wa utawala wa siasa wa nchi hii umekuwa ni mzunguko wa kudumu wa kutafuta kura. Unaomba kura na ukishapigiwa na kushinda unaanza tena kutafuta kura kwa kipindi cha miaka mitano. Ni maisha ya kura-kura-kura!

Katika mazingira ya namna hiyo, ni nani hasa anaweza kusema wanaotafuta kura wana nia ya dhati ya kuleta mabadiliko katika nchi hii? Kwamba ni kweli wanasukumwa na kiu na nia ya kutatua changamoto za kiuchumi za taifa hili, kwamba wanasumbuliwa na kuudhiwa sana na ufukara na umasikini wa watu wetu, na kwa maana hiyo wanataka sasa kujipanga kuachana na hali hiyo kwa haraka ili Tanzania iwe njema sana.

Ni wangapi kati ya wanaoomba kura wanasukumwa na kiu ya kutaka kubadili hali ya nchi yetu na siyo kujitwali madaraka ya mfumo wa viongozi kutawala wananchi na siyo kinyume chake. Mgeni Wicken aliliona hili mapema miaka ya sabini, leo tunaweza vipi kusema siyo?

Nchi hii itapiga hatua za maana za maendeleo iwapo tu tutatambua kuwa tumetekwa kwenye gulio kubwa la kura na mfumo wake ambao kwa sasa ni mzunguko wa miaka mitano, yaani maisha ya watu wetu sasa yametekwa kwenye uchaguzi.

Ni wachache sana wanasumbuliwa na kiu ya kweli ya kutaka kutatua kero na matatizo ya msingi ya taifa hili. Ukishaona taifa linalowaza uchaguzi wakati wote, basi jua tu, wananchi walishatekwa na wanasubiri tu vijizawadi ili watoe kura. Huu ni mkwamo mkubwa sana kwa taifa letu.

spot_img

Latest articles

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...

PURA yajivunia mafanikio katika Ajenda ya Nishati Safi na ushiriki wa Watanzania Sekta ya Mafuta na Gesi

Na Tatu Mohamed MAMLAKA ya Kudhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inajivunia...

More like this

Ndumbaro: Sheria 300 Zimetafsiriwa kwa Kiswahili Ili Kuimarisha Uelewa kwa Wananchi

Na Tatu Mohamed WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi...

Jessica: CCM inajali uongozi wa vijana

Na Mwandishi Wetu KATIBU wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM TAIFA, Jessica Mshama...

Waziri Aweso: Tuna uhakika wa maji ya kutosha Dar na Pwani

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewatoa hofu wakazi wa mikoa ya...