SIKU tatu za Mei 2023 yaani Jumatatu ya Mei 15, Mei 16 na Mei 17 zinabaki kuwa za kihistoria katika mapambano ya walipa kodi na wakusanya kodi katika nchi hii. Siku hizo tatu unaweza kuziita kielelezo cha malalamiko, manung’uniko, kero na mapambano ya walipa kodi dhidi ya wakusanya kodi ambao kwa miaka nenda rudi wamwekuwa na hulka ya kuamini kuwa kila mlipa kodi ni mjanja mjanja, na kwa maana hiyo ni lazima asakwe kama simba awindavyo swala nyikani.
Baadhi ya maduka yakiwa yamefungwa mitaa ya Kariakoo wakati wa mgomo huo.
Kwa nini tulifika hatua ya wafanyabiashara wa soko la kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam kufunga maduka yao? Kwa waliofuatilia kwa karibu mkutano wa ghafla wa kwanza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na wafanyabiashara Jumatatu ya Mei 15, 2023 walishughudia kilio cha wafanyabiashara kwa Mamlaka ya Mapato (TRA) ambao kwangu mimi nawaona kama wakusanya kodi tu kwani wajibu mwingine wa kulea na kusaidia kustawi wa biashara nchini wameutupa mkono.
Mkutano huu mwanzo Waziri Mkuu alikuwa na kazi ngumu, kutuliza ghadhabu za wafanyabiashara ambao walikuwa wamesitisha huduma zao kwa kufunga maduka kwa muda usiojulikana. Pamoja na juhudi hizo za siku ya kwanza, na pamoja na Waziri Mkuu kuomba kukutana na uwakilishi mpana zaidi wa wafanyabiashara kutoka mikoa yote nchini, hakufanikiwa kuwashawishi wafanyabiashara kufungua maduka yao kesho yake, yaani Mei 16, 2023.
Ni kweli, walimkubalia Waziri Mkuu kuwa wangefungua maduka, lakini kesho yake mitaa ya Kariakoo ilibakia kama mahame. Karibu maduka yote hayakufunguliwa. Wafanyabiashara hao walikuwa wanasubiri kuona nini kitatokea katika mkutano wa Jumatano Mei 17,2023 ambao ulikuwa ni mkutano mpana uliowakutanisha wafanyabiashara kutoka kona zote za nchi na watendaji wa serikali. Mkutano huo uliokuwa wa Waziri Mkuu na wafanyabishara pia ulihudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, makamishina wa TRA na watendaji wengine wakubwa serikalini.
Jambo la kukumbuka ni kwamba awali Jumatatu ya Mei 15,2023 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla sasa amehamishiwa Mwanza, alikuwa amejaribu kutuliza ghadhabu ya wafanyabiashara hao kwa kuwasihi wafungue maduka kwani Waziri Mkuu alikuwa amekubali kuonana nao ili kusikilia kero zao, hata hivyo alikwama. Hawakumkubalia. Waliendelea na mgomo. Waziri Mkuu aliibuka siku hiyo hiyo kujaribu kuokoa jahazi, lakini naye hakufanikiwa kuwabadili nia, ni mpaka alipokuja kuonana nao tena katika mkutano wa pili uliokuwa na uwakilishi mpana uliofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Wafanyabiashara hawa wana kilio kimoja. TRA. Kwamba watendaji wa mamlaka hiyo yenye dhima ya kukusanya kodi na kulea biashara nchini wamekuwa na tabia ya kudai rushwa, kuwabambika kodi kubwa na kukamata bidhaa zao mara kwa mara hata pale mwenye bidhaa husika amekuwa na uthibitisho wa stakabadhi ya mauzo au manunuzi ya bidhaa husika. Kwa kifupi kwa wafanyabiashara hawa TRA wamekuwa kama muumiani. Mwaka baada ya mwaka wanaibuka na mbinu mpya ya kufilisi wafanyabiashara kama kodi mpya ya stoo inayolalamikiwa sasa.
Lakini suala la kujiuliza ni hili, hivi ni nani hasa anajali hali hii? Kwamba ni mara ya kwanza kwa TRA kulalamikiwa juu ya maofisa wake kukiuka maadili ya kazi za ukusanyaji wa kodi? Kwamba si kweli malalamiko haya kila uchao yapo vinywani mwa wafanyabiashara na hata wawakilishi wa wananchi Bungeni; kwamba hata Marehemu Rais Dk. John Magufuli, pamoja na utawala wake kulaumiwa sana kwa kuwapa kiburi TRA alipata kuwalaumu kwa tabia yao ya kubambika wafanyabiashara makadirio makubwa ya kodi ili kujenga mazingira ya rushwa.
Wapo wafanyabiashara wanasema wazi kabisa mfumo wa kodi katika nchi yetu siyo rafiki kabisa, makadirio yake siyo rafiki na hayazingatii mazingira halisi ya biashara ndani ya nchi na hata nje ya nchi. Wanasema hali iliyoko ni kama vile maofisa wa TRA wanaishi nchi ua dunia ya kusadikika halafu wanakuja Tanzania kukadiria na kukusanya kodi bila kuyaelewa mazingira halisi ya kufanya biashara nchini.
Kwa mfano, katika malalamiko ya wafanyabiashara ni kwamba ni rahisi kununua bidhaa za nguo kama vitenge na mashuka kutoka Zambia na Uganda ambao huagiza mizigo hiyo kutoka nje, kuliko mfanyabiashara wa Kitanzania kuagiza mizigo hiyo hiyo kutoka China, India, Uturuki na kwingineko. Yaani, wakati Tanzania ina bandari na gharama za kusafirisha mizigo ni rahisi kuliko Zambia na Uganda ambao mbali ya kulipia gharama za bandarini hapa nchini, pia husafirisha kwa barabara au reli mpaka kwao, bado bidhaa ndani ya nchi yao ni rahisi kuliko hapa nchini. Na ni faida zaidi Mtanzania kwenda kununua bidhaa hizo huko Zambia na Uganda, kuliko kuagiza mwenyewe kutoka nje. Kwa kifupi kodi za Tanzania hazilipiki. Ni kubwa mno, hazitabiriki, hakuna uwazi na hazizingatii hali halisi ya biashara humu nchini na hata huko nje.
Katika mazingira haya mtu anajiuliza, hivi katika nchi hii nani hasa anajali? Hivi Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba ambaye alipata kuwakejeli Watanzania wanaohoji tozo wahamie Burundi, au wabunge wanaohoji mambo ya uchumi kuachana na hoja zao kwani wao wanaweza mambo ya uganga wa kienyeji, ni Waziri anayeweza kutambua nini cha kufanya ili Tanzania iwe mshindani katika biashara ya ndani na hata ya nje?
Ni jambo la bahati mbaya sana siku hizi, nafasi ya Waziri wa Fedha na hata Katibu Mkuu wake zimerahisishwa sana kiasi kwamba yeyote tu anaweza kuteuliwa kushika nafasi hizo. Lakini kwa kweli kwa wanaoifahamu nchi hii vema, nafasi ya Waziri wa Fedha na Katibu Mkuu wake ni nafasi nyeti pengine kuliko zote katika taifa hili kwa kuzingatia ustawi wa nchi na watu wake.
Tunakumbuka miaka ya 90 mwanzoni Tanzania ilipata kusimamishiwa misaada na nchi washirika wakati huo Waziri wa Fedha akiwa Profesa Kighoma Malima. Tanzania ilishindwa kukusanya kodi, wakati hiyo ilishindwa kukusanya Sh. bilioni 70. Zilikuwa ni fedha nyingi sana wakati huo. Hali hiyo iliparaganya kabisa uchumi. Rais Ali Hassan Mwinyi baada ya shinikizo kubwa alimundoa Profesa Malima katika nafasi hiyo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisikiliza kero za wafanyabiashara Mei 17,mwaka huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Leo, tunazungumza jeuri, kiburi na ujivuni wa maofisa wa TRA kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili tunaona kibri na jeuri ya Waziri Mwigulu Mchemba katika kusimamia sekta ya fedha. Waziri anayejigamba kwamba ni msomi wa uchumi aliyebobea, Waziri anayetamba kwa kuonyesha vyeti vyake vya elimu na kukataa kusikiliza sauti yoyote ambayo haikubaliani naye kuhusu sera za fedha na kodi, hata kama inaonekana dhahiri zinaumiza sekta ya biashara nchini.
Jaribu kujiuliza baada ya mnyukano baina ya wafanyabiashara na watendaji wa serikali katika mkutano na Waziri Mkuu, Mwigulu wala hakuona kuna jambo la kumshitua ndiyo maana baada ya mkutano badala ya kuwa ameelemewa na mambo kwa jinsi malalamiko ya wafanyabiashara yalikuwa mazito na kuonekana jinsi TRA ilivyojaa watu waovu, yeye aliona ni wakati wa kujipiga selfie na wafanyabiashara. Yaani Mwiguli anajiona yeye ni ‘celebrate’ fulani hivi. Hakosi usingizi kwa sababu ya malalamiko, kero na shida za wafanyabiashara wanaofilisiwa na TRA kwa makusudi kwa kuendesha ukusanyaji wa kodi usiorafiki.
Jaribu kufikiria na kujiuliza, katika mazingira ya kusimama kwa soko la kimataifa la biashara la Kariakoo kwa siku tatu mfululizo, hasara ambayo serikali imepata kwa kutokupata kodi kwa siku hizo, hivi Waziri wa Fedha timamu anapata wapi ujasiri hata wa kutabasamu achilia mbali kupiga selfie na watu huku meno 32 yakiwa nje yote. Hii furaha anaipata wapi? Je, aliingiwa na chochote kichwani katika malalamiko ya wafanyabiashara katika mkutano huo.
Je, ni kweli malalamiko yale yalikuwa ni mapya kwa Mwigulu siku ile? Hakika angekuwa ni mtu anayekosa usingizi kwa sababu ya dhima aliyobeba, Jumatano ya Mei 17, 2023 ilipaswa kuwa siku ya giza nene, machungu na huzuni kubwa kwa Mwigulu, lakini kwa wanaosoma nyuso za watu – paralinguistics gestures Mwigulu ni yule yule wa hamieni Burundi kama hamtaki tozo!