Legacy kwa gharama yoyote inatugarimu

Na Jesse Kwayu

KAZI ya kuandikisha wapiga kura kwa mfumo mpya wa kieletroniki wa kutambua viungo vya mwili (yaani biometric voter registration (BVR) kwa madhumuni ya kupata daftari la wapiga kura kwa ajili ya kura ya maoni ifikapo Aprili 30, mwaka huu na upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu, inaendelea katika mkoa wa Njombe.

Uandikishaji huo tangu uanze Februari 23, mwaka huu leo (Machi 18) unaingia siku ya 21 ya kuandikisha. Idadi ya siku hizo ni baada ya kuoandoa siku tatu za Jumapili ambazo uandikishaji haufanyiki.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imenukuliwa ikisema kuwa kazi ya kuandikisha mkaoni Njombe itaendelea hadi Aprili 12 mwaka huu. Kwa maana hiyo NEC itakuwa imejichimbia Njombe kwa takriban siku 49, lakini za kazi zikiwa ni 42.

Taarifa kutoka NEC zinasema kuwa hadi sasa wana BVR 250 tu. Tangu uandikishaji uanze Njombe BVR zilizokuwa zinatumika ni pungufu ya 250 na hadi wiki hii inaanza ndipo ripoti ilitolewa kwamba sasa BVR zote 250 zimepelekwa Njombe.

NEC imekuwa inasema kuwa imeagiza BVR nyingine takribani 3,000 na zipo njiani. Kauli hii kwamba BVR nyingine zimekwisha kuagizwa imekuwa ikirejewa mara kadhaa na uongozi wa juu wa NEC, lakini siku zinaendelea kukatika bila kuwasili.

Tanzania ina mikoa 30, kwa maana hiyo kama uandikishaji wa wapiga kura mkoani Njombe utakamilika Aprili 12, mwaka huu ina maana kwamba zitakuwa zimebakia siku 18 kufikia Aprili 30, siku ambayo serikali imepanga kuwa ya kupiga kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa.

Inawezekana kabisa NEC ikafanya uandikishaji kwa kasi kubwa zaidi katika mikoa 29 iliyobaki kwa kwa sababu labda itakuwa imepata BVR za kutosha, kwa maana hiyo kusambaa mikoa yote kwa mpigo. Hilo kimahesabu linawezekana.

Uwezekano huo ni kama NEC ingelikuwa na BVR za kusambaza kila mkoa kwa wakati mmoja ili kazi hiyo ifanyike kwa wakati mmoja. Tangua sasa hadi Aprili 30, mwaka huu kuna siku 43. Siku hizo ukiondoa siku sita za Jumapili, kazi hiyo itafanyika kwa siku 37 tu nchi nzima.

Katika mfumo wa kazi ambao hauna vikwazo, siku 37 za kufanya kazi ni nyingi, lakini katika mfumo unaoelezwa kuwa mpya, wenye changamoto nyingi za kiweledi na kitekinolojia bila kusahau jiografia ya nchi, siku 37 ni chache sana.

Mbali na kuandikisha wapiga kura kuna kazi ya uhakiki wapiga kura. Je, kazi hiyo itafinyika katika uandikishaji wa safari hii au la? Na kama kuna kuhakiki, ina maana uandikishaji utakwenda sambamba na kampeni za kura ya maoni?

Kila anayetafakari ratiba hii kuelekea kura ya maoni na shinikizo la uandikishaji uwe umekamilika mapema kabla ya Aprili 30, mwaka huu, anajikuta akiibuka na maswali magumu ambayo majibu nayo hayapatikani. Kwamba haraka yote hii ni ya nini?

Juzi Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro, wakati wa hafla ya kukabidhi nakala ya Katiba iliyopendekezwa kwa makundi mbalimbali yatakayoshiriki kutoa elimu ya uraia kuhusu katiba hiyo, alisema hadi sasa hakuna mabadiliko juu ya tarehe ya kura ya maoni.

Aliongeza kuwa ratiba inaendelea kama ilivyopangwa, hata hivyo alisema kama wakipata ushauri kutoka kwa NEC juu ya mchakato mzima wa uandikishaji, serikali itakaa na kuangalia cha kufanya kulingana na ushauri huo.

Tangu Bunge Maalum la Katiba lilipokuwa linaendelea na kazi ya kuandaa katiba inayopendekezwa mwaka jana, kumekuwa na maoni ya wadau mbalimbali juu ya muda mwafaka wa kupigwa kwa kura ya maoni.

Kuna wakati Rais Jakaya Kikwete alikutana na wawakilishi wa vyama vya siasa chini ya mwavuli wa Kituo cha Demokrasia (TCD) na kukubaliana kwamba kura ya maoni ingepigwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Kwa maneno mengine serikali ya awamu ya tano ndiyo ingelikuwa na jukumu la kusimamia kura hiyo.

Hata hivyo, makubaliano hayo ambayo yalitangwa na viongozi wa kisiasa waliohudhuria mazungumzo ya rais na wanasiasa hao, yalitupiliwa mbali na kilichoendelea ni mchakato ambao umebananisha mambo kati ya Januari mwaka huu na Aprili mwaka huu.

Ukiacha wanasiasa, ukiwasikia baadhi ya makamishna wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, unapata picha ile ile kwamba mchakato wa kufikiwa kwa kura ya maoni usingeliwezekana kufanyika Aprili mwaka huu. Sababu kubwa ambayo imekuwa ikitolewa ni kutokuwapo kwa muda wa kutosha wa maandalizi ya kura hiyo, hasa suala la uandikishaji wa wapiga kura katika daftari la wapiga kura kwa mfumo wa BVR na elimu ya urais juu ya katiba pendekezwa.

Kwa nyakati tofauti nimekuwa na fursa ya kukutana na wachambuzi wa siasa katika matukio tofauti, miongoni mwa mambo mengine ambayo wamekuwa wakichambua ni uharaka wa kura ya maoni.

Wengi wamekuwa na mawazo chanya kuhusu kura ya maoni, wengine hata kusema kuwa katiba inayopendekezwa pamoja na kuchakachuliwa kwa maana ya kutupwa baadhi ya mapendelezo muhimu kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hususan, maadili ya viongozi na uwajibikaji, bado ina mambo ya maana yanayopendekezwa ingawa hayajafikia asilimia 100 kama ilivyokuwa kwenye mapendekezo ya Tume.

Kinachowasumbua wachambuzi na wanazuoni hawa ni je, ni sawa serikali ya awamu ya nne kuchukulia suala la kura ya maoni kama jambo la kufa au kupona? Je, ikiacha mchakato wa kura ya maoni kuendeshwa na awamu itakayoingia madarakani baada ya Oktoba mwaka huu, kutakuwa na tatizo gani?

Wanazuoni hawa pamoja na misimamo yao inayokinzana katika mambo mengi na ubora wa katiba inayopendekezwa, wanasema kuwa kinachosumbua serikali ya awamu ya nne ni ‘legacy’. Yaani urithi, au hiba. Awamu ya nne imeamua kwamba yenyewe ichukue sifa au pongezi za kuwa serikali iliyoanzisha, ikasimamia na kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wanazuoni hao wanasema kuwa ingawa ni haki ya kila awamu ya utawala kutaka kuacha urithi wake kwa vizazi vinavyofuata, ni kupotoka kudhani kwamba kila kitu kinapimwa kwa nyakati au vipindi vifupi vifupi vya miaka mitano au 10.

Mathalan, mtu akitaka kuzungumzia kustawi na kuendelea kuwako kwa amani na utulivu nchini, ni awamu gani hasa inaweza kujitwalia haki ya kuwa na hati miliki ya hali hiyo? Hali hii ilinifanya nifikiri kwa kina zaidi.

Kwa jinsi hali inavyokwenda shinikizo la kura ya maoni inaakisi kile kile kilichojitokeza wakati wa majadiliano ndani ya Bunge Maalum la Katiba. Kwamba kile kilichokuwa kinatakiwa na serikali na kwa maana hiyo chama tawala, ndicho kilipatikana hata kama wananchi walikuwa wanataka tofauti na hivyo.

Hali hii inaashiria nini? Kwamba kila uchao kinachoonekana siyo tu kuaharakia kupata katiba mpya, bali kiu kiu ya kuacha legacy. Bahati mbaya mwelekeo huo wa mambo unadhihirisha ubinafsi wa kutaka mimi tu na siyo mwingine.

Shikinizo hizo zikitazamwa kwa kina zaidi zinatoa picha ambayo inaonyesha kwamba huenda Tanzania itakoma kuwako baada ya awamu ya nne kumaliza muda wake hapo Oktoba mwaka huu. Fikra hizi zinajithihirisha kwa jinsi watawala wamejaza pamba masikioni mwao kiasi cha kukataa kusikiliza chochote kutoka kwa yeyote ambaye haimbi wimbo wao wa kura ya maoni Aprili 30.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba ingawa kila mwanasiasa anataka kuacha kumbukumbu yake nyakati zake za kuongoza, ni vema pia matamanio hayo yakatazamwa katika sura ya kujenga ustawi wa taifa. Legacy siyo kitu cha kibinafsi, siyo kitu cha awamu, ni kitu kinacholenga kusaidia taifa na watu wake kwa manufaa ya kitaifa zaidi.

Ni bahati mbaya kwamba suala la katiba mpya tangu awali limeondolewa kwenye reli yake kuwa kitu cha makubaliano na maridhiano ya kitaifa yanayolenga kutambua mahitaji, hisia, uzoefu na matarajio ya kila mmoja katika taifa, kuwa kitu cha kikundi kimoja katika jamii chenye nia ya kuacha legacy bila kujali kwamba kufanya hivyo wanaacha nyufa nyingi zaidi ndani ya taifa kuliko kujenga. Ni katika kutazama hisia na matarajio ya watawala wa sasa, mtu anashindwa kukwepa hitimisho kwamba kinachosumbua NEC na uandikishaji huu wa kufa au kupona, uandikishaji huu wa kung’ang’ana kwamba ije mvua au jua kali, ni lazima kura ya maoni ipigwe Aprili 30, mwaka huu, jibu la yote haya ni kiu ya legacy kwa gharama yoyote

spot_img

Latest articles

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...

Watu wawili wafariki, 16 wajeruhiwa katika ajali ya basi Songwe

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Watu wawili wamefariki dunia na wengine 16 kujeruhiwa baada ya...

More like this

Soma Ripoti ya UHIFADHI WA UHAI: UKIUKWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NDANI YA SEKTA YA UHIFADHI TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Media Brains Utafiti mpya umebaini kwamba mamlaka za serikali zimekuwa kichocheo kikuu...

RAIS DKT. SAMIA ATOA MAAGIZO KWA BASHE, NFRA KUNUNUA MAHINDI KWA WAKULIMA TSH 700 KWA KILO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassanamemuagiza Waziri wa Kilimo...

Upi upepo unaoweza kufika Tanzania,wa Wiliam Ruto au Paul Kagame?

KUNA upepo wa aina mbili unavuma katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mmoja...