Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imesema ushindi wa nafasi ya tatu ilioupata katika kundi la taasisi za elimu ya juu na uendelezaji ujuzi kwenye Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ni uthibitisho wa imani kubwa ambayo wananchi wameendelea kuionesha kwa huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.
Akizungumza baada ya kuhitimishwa kwa maonyesho hayo, Meneja wa Uhusiano wa VETA, Sitta Peter, aliwashukuru Watanzania waliotembelea banda la mamlaka hiyo na kujionea shughuli mbalimbali za mafunzo, ubunifu na utafiti zinazotekelezwa.

“Tunamshukuru Mungu na kuwashukuru Watanzania wote waliotembelea banda letu. Maonesho haya yalikuwa fursa muhimu ya kutoa elimu kuhusu mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ubunifu na teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa na VETA kwa ajili ya kutatua changamoto za jamii,” alisema Sitta.
Alisema tuzo waliyoipata katika maonyesho hayo ni motisha kwa VETA kuendelea kuboresha mafunzo, tafiti, ubunifu na bidhaa zinazozalishwa ili ziendelee kukidhi mahitaji ya wananchi na soko la ajira.
“Tuzo hii inaonyesha wananchi wanatambua na kuthamini kazi inayofanywa na VETA. Sisi tutaendelea kuboresha huduma zetu, ubunifu wetu na bidhaa zetu ili ziwe na mchango mkubwa zaidi kwa maendeleo ya nchi,” alisema.

Alifafanua kuwa, VETA imeendelea kufanya tafiti zinazojikita katika mahitaji halisi ya jamii, ambapo matokeo yake yamekuwa yakizalisha teknolojia, bidhaa na ubunifu unaosaidia kutatua changamoto mbalimbali za wananchi.
“Utafiti wetu unalenga matumizi ya moja kwa moja kwenye jamii. Kila ubunifu unaouona kwenye banda letu umetokana na kutafiti changamoto zilizopo na kutafuta suluhisho lake. Hivyo tunaendelea kubuni teknolojia zinazogusa maisha ya wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa pamoja na kutoa mafunzo ya ufundi stadi, VETA pia imeendelea kufanya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupitia vyuo vyake, hatua inayochangia kuongeza mapato ya taasisi na kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.

Sitta alitoa wito kwa wananchi, hususan vijana, kuyapa kipaumbele mafunzo ya ufundi stadi akieleza kuwa ndiyo suluhisho la changamoto ya ajira na msingi muhimu wa kukuza uchumi wa taifa.
“Mafunzo ya ufundi stadi ni mkombozi wa ajira kwa vijana na ndiyo nguzo muhimu ya kusukuma uchumi wa nchi. Tunawaomba wananchi wayape kipaumbele kwa sababu yanawawezesha kujiajiri na kuajiri wengine,” alisema.
Akizungumzia mchango wa VETA katika ukuaji wa biashara, Sitta alisema taasisi hiyo ina nafasi kubwa katika kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi, ambayo ndiyo msingi wa uzalishaji na maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.


