Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua Nyumba Janja yenye mfumo wa kisasa wa teknolojia unaosaidia kuongeza usalama wa nyumba kwa kupunguza hatari za majanga kama moto na ajali nyingine zinazosababishwa na hitilafu za umeme.
Nyumba hiyo, ambayo ni moja ya vivutio vikubwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba, imeundwa kwa teknolojia inayorahisisha matumizi ya umeme kwa kumwezesha mtumiaji kudhibiti vifaa mbalimbali vya umeme kupitia programu maalumu ya simu akiwa popote duniani.
Akizungumza katika banda la TANESCO, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa shirika hilo, Irene Gowele, alisema teknolojia hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya umeme na kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwawezesha kutumia umeme kwa njia ya kisasa na salama.

Alisema kupitia mfumo huo, mtumiaji anaweza kuwasha au kuzima vifaa vya umeme akiwa mahali popote, sambamba na kufuatilia kiwango cha umeme kinachotumiwa na kila kifaa ili kupunguza gharama za matumizi.
“Teknolojia hii inawasaidia wateja kudhibiti matumizi ya umeme kwa ufanisi zaidi. Pia ndani ya Nyumba Janja tumeweka vifaa vinavyotumia umeme kwa ufanisi (energy efficient appliances), ambavyo vinatumia umeme kidogo lakini vinatoa huduma bora,” alisema Gowele.

Mbali na kuonesha teknolojia ya Nyumba Janja, TANESCO inaendelea kutekeleza mpango wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuuza majiko ya umeme kwa njia ya mkopo.
Gowele alisema wananchi wanaotembelea banda la TANESCO katika maonesho hayo wanaweza kununua au kukopa majiko hayo kwa kuwasilisha namba ya mita ya umeme pamoja na Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIDA) kwa ajili ya kuthibitisha taarifa zao kama wateja wa TANESCO.

Alieleza kuwa majiko hayo yanatumia umeme kidogo na yana uwezo wa kupika aina mbalimbali za vyakula vya Kitanzania kwa gharama nafuu, hivyo kusaidia kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira.
Aidha, alisema TANESCO imetumia teknolojia ya kidijitali kuwawezesha wananchi kujionea baadhi ya miradi mikubwa ya uzalishaji umeme nchini, ikiwemo Kituo cha Kufua Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) na mradi mkubwa wa kwanza wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jua uliopo Kishapu mkoani Shinyanga wenye uwezo wa kuzalisha megawati 50.
Pia shirika hilo linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, ikiwemo magari na bajaji za umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na teknolojia rafiki kwa mazingira.



