Na Tatu Mohamed
WANAFUNZI wanaosoma mkondo wa amali wameanza kuonesha matokeo ya ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri na kutimiza ndoto zao za kitaaluma, huku Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) likitumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kuonesha mafanikio ya utekelezaji wa mfumo huo.
Kupitia banda la NACTVET, wananchi wameshuhudia wanafunzi wakifanya kazi mbalimbali za umeme, kuchora ramani za majengo na kuwasilisha miradi ya ubunifu, jambo linaloonesha namna maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023, yalivyoanza kuzaa matunda.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 2, 2026, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa NACTVET, Dora Tesha, amesema lengo la kuwashirikisha wanafunzi kwenye maonesho hayo ni kuwapa wananchi nafasi ya kujionea uwezo wanaoupata kupitia mkondo wa amali.
“Tunataka wazazi na wananchi wajionee kuwa elimu ya amali si nadharia pekee. Wanafunzi hawa wana uwezo wa kufanya kazi za umeme, kuchora ramani za majengo na kutengeneza miradi mbalimbali. Haya ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika elimu ya amali,” amesema Tesha.
Ameongeza kuwa, NACTVET inaendelea kusimamia ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kujiajiri.
Mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Baobab, Careen Jonathan Maky, anayesomea fani ya umeme, alisema mkondo wa amali umembadilishia mtazamo kwa kumpa ujuzi wa vitendo na kuimarisha ndoto yake ya kuwa mhandisi.

Naye mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru, Daud Elias, amesema mafunzo hayo yamemwezesha kujifunza kuchora ramani za majengo na kuelewa hatua mbalimbali za ujenzi, akieleza kuwa kuendelea kuimarishwa kwa mkondo wa amali kutazalisha kizazi cha vijana wenye ujuzi kitakachochochea maendeleo ya uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, mwalimu wa taaluma ya amali katika Shule ya Sekondari Baobab, Philip Lazaro, alisema mfumo huo unawajengea wanafunzi uwezo wa kuanzisha shughuli za kiuchumi mara baada ya kuhitimu badala ya kusubiri ajira rasmi.



