MEI mwaka huu picha mjongeo ya mahojiano kati ya Inspekta Jenerali wa Polisi Mstaafu, Omar Mahita na M&S Podcast, ilisambaa kama moto wa nyika kwenye mitandano ya kijamii. Pengine kikubwa kilichosababisha hali hiyo ni mada alizozungumza IGP Mstaafu Mahita. Mahita alitumika kama IGP kuanzia Mei 1996 hadi Machi 2006, wakati wote wa utawala wa Rais Benjamin Mkapa. Aliondoka madarakani wakati utawala wa Rais Jakaya Kikwete ukiwa na umri wa miezi minne hivi.
Katika mahojiano hayo IGP Mahita anaonekana kuongea kwa kujiamini kama ilivyo ada yake, amezungumzia mambo mengi. Kubwa ambalo linanisukuma kumkumbuka leo ni kauli yake kwamba IGP hapaswi kupokea maelekezo ya kisiasa kuhusu utekelezaji wa kazi za kipolisi, isipokuwa kutoka kwa viongozi wakuu wa kikatiba katika mipaka ya mamlaka yao.
Alisisitiza kuwa kuna changamoto kubwa kwa Jeshi la Polisi la sasa kuingiliwa na wanasiasa, kwani polisi mwenye weledi hapaswi kuruhusu maamuzi yake ya kitaaluma yaamuliwe na shinikizo la kisiasa. Alifafanua kuwa Jeshi la Polisi lina mfumo wake wa uongozi na linaweza kujiendesha kitaaluma bila kuhitaji kuingiliwa katika maamuzi ya kila siku ya kiutendaji na viongozi wa kisiasa.
Maagizo ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi kwa IGP Camillius Wambura aliyoyatoa bungeni wiki iliyopita ya kumtaka kuzuia/kusitisha kwa muda mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa nchini kwa sasa, ndiyo hasa yamesababisha kuyakumbuka mahojiano ya IGP Mahita na M&S Podcast.
Katambi katika tamko lake ambalo limepingwa na wadau wengi wa haki za binadamu, wanaharakati na wanasiasa, alieleza linatokana na sababu za kiusalama, si kwa lengo la kuondoa demokrasia. Aliainisha sababu hizo kuwa ni kuwepo kwa viashiria vya uchochezi, ambavyo anadai vinaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi; na tishio la maandamano. Alisema marufuku hiyo inahusu vyama vyote vya siasa, vikiwemo chama tawala na vyama vya upinzani, na kwamba ni hatua ya muda hadi itakapotolewa taarifa nyingine.
Kumekuwa na hoja mujarabu kwamba Katambi anapata wapi mamlaka ya kuharamisha haki za binadamu ambazo zimeainishwa wazi kwenye katiba? Je, Katambi anayo mamlaka ya kuamrisha tu Jeshi la Polisi lifanye jambo fulani la kiutendaji ambalo kimsingi ni wajibu wa kitaaluma wa Jeshi hilo?
Ukimsikiliza Katambi kwa umakini zaidi, anatoa ya moyoni mwake, kwamba tayari kuna watu wamekamatwa wakiwa na madumu ya petroli; wapo waliokamatwa na silaha; na wapo wanaopanga mikakati ya uhalifu. Kwa maana hiyo, kama kuna watu wanafanya vitu hivyo, eti itakuwa ni vigumu kuwakamata katika mikusanyiko! Hivyo, dawa ni kusitisha mikutano ya hadhara ili kuwasaka.
Katambi anapiga hatua nyingine kwamba wananchi waachwe wafanye kazi za kujenga uchumi
wao; kwamba wafanyabiashara na wawekezaji wapewe fursa ya kutekeleza shughuli zao bila bugudha.
Ya Katambi siyo mapya. Amekumbuka chupa ya divai iliyokuwa imefichwa kabatini. Hii ni chupa aliyoizundua Marehemu Rais John Magufuli mwaka 2016 baada ya kuingia madarakani mwaka 2015. Alisimamisha shughuli za mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya upinzani. Sababu kubwa aliyoitoa ni ili kuwaacha wananchi wafanye shughuli za kiuchumi. Mantiki inayopatikana hapa ni kwamba shughuli za kisiasa zinapora wananchi fursa ya kufanya shughuli za kiuchumi. Katambi amekumbuka mvinyo huo na sasa anataka kuwanywesha tena Watanzania.
Kisingizio hiki kilichoasisiwa wakati huo bila shaka ndicho kinatajwa kuwa mojawapo ya sababu ya yale yalitokea Oktoba 29, 2025. Ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya Jaji Mohamed Chande kuhusu matukio ya vurugu za baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ilitaja kuminywa kwa uhuru wa kisiasa kama moja ya changamoto/vichocheo vilivyohusishwa na muktadha wa matukio hayo.
Haya ni malalamiko kuhusu mifumo ya kisiasa na ushiriki wa vyama vya siasa, hoja za haki za kiraia na uhuru wa kujieleza/kukusanyika na madai ya upungufu katika mazingira ya demokrasia na uwakilishi wa kisiasa. Hali hii ilijenga kidogokidogo hali ya kukata tamaa na hasira ndani ya jamii, kiasi kwamba yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na baada yake yana mzizi huko.
Katambi ni mwanasiasa. Amepata kuwa upande wa upinzani. Anajua fika jinsi uwanja wa kisiasa nchini usivyotoa fursa sawa kwa vyama vyote vya siasa. Katambi anajua wazi haya, hiyo marufuku anayomtaka IGP Wambura aitekeleze walengwa hawawezi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Analijua vema hili. Anajua CCM haijawahi kuzuiwa kokote. Anajua CCM ni chama dola. Anajua hata kwenye wavaaji wa sare (men and women in uniforms) ndani yake wapo wenye mapenzi na chama tawala. Kwa maneno machache, marufuku ya Katambi ni jiwe limerushwa gizani huku akiwa ameshikilia tochi ili limtie ngeu fulani – mlengwa!
Hata hivyo, tupige hatua kidogo. Yaani kwa hali ambayo taifa linapitia, ndani na nje ya nchi, tangazo la Katambi linajenga au linazidi kubomoa? Kwamba hata baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, hata katika kilio cha miaka yote hii cha watu kutekwa, kupotezwa na wengine kuuawa hadharani, Katambi anaamini haya yake ndiyo maarifa ya kuponya taifa?
Hakuna mtu yeyote katika nchi hii anashurutishwa ama kujiunga na chama cha siasa au kushiriki shughuli za vyama vya siasa kiasi cha kuhisiwa kwamba eti wananchi wanapotezewa muda wao wa kufanya shughuli za kiuchumi kisa mikutano ya hadhara. Mkulima haisubiri serikali au mtu yeyote kumwambia kuwa sasa ni msimu wa kulima, kupalilia au kuvuna; vivyo hivyo mfanyabiashara hahitaji kukumbushwa na yeyote muda wa kufanya shughuli zake. Nchi hii hakuna anayeshurutishwa kufanya kazi wala kujiunga na shughuli za kisiasa. Hivyo, hoja ya eti wananchi waachwe wafanye shughuli zao, haina msingi wowote.
Katambi kama ambavyo walivyo wengine wengi wenye nafasi katika nchi hii, bado hawataki kukubaliana na ukweli kwamba kama taifa tuna tatizo kubwa sana la kisiasa. Kidogo kidogo tuliamini kwamba unaweza kujenga kukubalika kwa wananchi kisiasa kwa kutumia polisi. Kwamba matukio ya Oktoba 29, 2025 hayajatusaidia kujitambua na kwa maana hiyo turejee kwenye mstari ili kuitibu nchi. Tungali tunasaka mchawi wa kukataa kuukubali ukweli kwamba tumeharibu nchi. Kwa staili ya Katambi na tuhuma za kuumbaumba tunatengeneza janga lingine kubwa zaidi.


