Na Mwandishi Wetu
Zaidi ya waogeleaji 400 wenye umri wa miaka 6 hadi 12 wanatarajiwa kushiriki Mashindano ya vilabu kwa nchi za Afrika Mashariki yatakayofanyika kuanzia kesho Juni 6 hadi 7, 2026 katika bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), Masaki jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, Mkurugenzi wa Elimu na Maendeleo wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Jeremiah Keema amesema mashindano hayo yatashirikisha jumla ya vilabu 25 kutoka nchi nne ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia.
Keema amesema mashindano hayo yanalenga kuwapa waogeleaji chipukizi nafasi ya kuonesha vipaji vyao, kujenga uzoefu wa ushindani wa kimataifa na kuimarisha mahusiano ya michezo kati ya nchi zinazoshiriki.
Aidha, amebainisha kuwa mashindano hayo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza mchezo wa kuogelea kwa vijana na kuandaa kizazi cha waogeleaji watakaoiwakilisha vyema Tanzania katika mashindano ya ngazi mbalimbali siku zijazo.


