Na Winfrida Mtoi
JUMLA ya waogeleaji 19 wamekabidhiwa bendera Mei 2, 2026 kwenda kuiwakilisha Tanzania katika Mashindano ya 17 ya Kuogelea ya Afrika, yatakayofanyika nchini Algeria kuanzia Mei 5 hadi 13,2026.
Mashindano hayo yatahusisha makundi mbalimbali yakiwemo timu ya vijana ‘junior team’, timu ya wakubwa ‘senior team’ pamoja na kundi la wachezaji wenye umri mkubwa ‘masters.
Akizungumza wakati wa kukabidhi bendera kwa timu hiyo katika bwawa la kuogelea Shaban Robert jijini Dar es Salaam, Ofisa Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, amewataka waogeleaji hao kutambua kuwa wameibeba Tanzania, hivyo wajitoe kwa dhati kuhakikisha wanashinda.


“Serikali ipo nyuma yenu na uongozi wa TSA (Chama cha Kuogelea Tanzania), wazazi na watanzania wote wapo nyuma yenu kuhakikisha mnakwenda kufanya vizuri,” amesema.
Aidha amewaomba Watanzania wanaoishi nchini Argeria kujitokeza katika mashindano hayo ili kuipa sapoti timu hiyo wakati ikichuana.
Naye Mwenyekiti wa TSA, David Mwansyoge, amesema malengo walitojiwekea ni kufika fainali ya mashindano hayo, huku akiishukuru Serikali na wazazi kutokana na kujitoa katika kufanikisha safari hiyo.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TSA, Amina Mfaume, ameeleza kuwa kati wachezaji hao 19, ‘junior team’ wapo 14, senior watatu na masters wawili. ” Wachezaji wote wamefanya mazoezi ya kutosha tunaamini watafanya vizuri,”
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha wa timu, Filbertha Demelo amesema wamejindaa vyakutosha na wanakwenda Algeria kupambana ili kufanya vizuri.


