Dkt. Mataragio: Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wanaoficha mafuta

Na Tatu Mohamed

SERIKALI imetoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na vitendo vya kuficha mafuta kwa lengo la kuyauza kwa bei ya juu baadaye, ikisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuvuruga utaratibu wa soko.

Akizungumza wakati wa ziara katika maghala ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni ya Camel Oil yaliyopo Kurasini, jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unabaki thabiti nchini.

Amesema ziara hiyo imelenga kujionea hali halisi ya akiba ya mafuta na mwenendo wa usambazaji wake kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya vituo vya mafuta vinavyodai kucheleweshewa huduma.

“Tumesikia kelele kwamba kuna baadhi ya vituo havipati mafuta kwa wakati au kuna ucheleweshaji wa makusudi katika upakiaji. Serikali haitavumilia hali hiyo,” amesema Mataragio.

Ameeleza kuwa kwa sasa hakuna uhaba wa mafuta nchini na akiba iliyopo inatosha kukidhi mahitaji ya wananchi kwa miezi kadhaa ijayo, akisisitiza kuwa hofu miongoni mwa wafanyabiashara na wananchi ndiyo inayochangia kuonekana kwa uhaba usio wa kweli.

“Sisi Serikali tunawahakikishia Watanzania kwamba mafuta yapo ya kutosha, hivyo hakuna sababu ya kununua kwa wingi au kuficha,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Mataragio ameipongeza Kampuni ya Camel Oil kwa kuendelea kutoa huduma saa 24, akiwataka wadau wengine wa sekta hiyo kuiga mfano huo ili kuhakikisha usambazaji unakuwa wa uhakika wakati wote.

Amegusia pia athari za mvutano unaoendelea katika ukanda wa Mashariki ya Kati, akisema umeathiri soko la mafuta duniani, lakini Tanzania imechukua hatua za mapema kudhibiti athari hizo na kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unabaki salama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile, amesema changamoto za soko la dunia zinatokana na utegemezi mkubwa wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati.

Amefafanua kuwa pamoja na changamoto hizo, Serikali imefanikiwa kuweka mazingira mazuri ya uagizaji na usambazaji wa mafuta nchini.

“Hakuna uhaba wa mafuta kwa sasa, ingawa gharama za uagizaji zinaweza kuongezeka kutokana na mabadiliko ya soko la dunia,” amesema Andilile.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Camel Oil, Saleh Bajber, amesema kampuni hiyo ina akiba ya kutosha ya mafuta na inaendelea kusambaza bidhaa hiyo bila kukwama.

Ameeleza kuwa kampuni hiyo imeagiza zaidi ya lita milioni 70 kwa mwezi Aprili na inatarajia kuingiza lita milioni 84 mwezi Mei, huku tayari ikiwa imesambaza zaidi ya lita milioni 44 hadi Machi 25, 2026.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wasambazaji wa Mafuta nchini (Tapsoa), Augustino Mmasi, amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo umeimarisha upatikanaji wa mafuta nchini.

“Nawafahamisha wafanyabiashara na wananchi kuwa mafuta yapo ya kutosha. Tumeendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha usambazaji unakuwa wa uhakika,” amesema Mmasi.

spot_img

Latest articles

Matendo ya Polisi ni hujuma dhidi ya utawala bora, demokrasia

MFUMO wa uchumi wa soko huru una kanuni zake. Miongoni mwake ni kuruhusu ushindani....

Lukuvi afariki dunia

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye...

Mgodi wa kihistoria wa niobium kujengwa Mbeya

Na Mwandishi Mbeya TANZANIA imepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Marekani baada...

Ndejembi ataka Ewura kukagua maghala ya mafuta kuhakikisha hakuna mafuta yanayofichwa

📌Asema nchi ina usalama mkubwa wa mafuta hivyo wananchi waendelee kupata huduma muda wote 📌Timu...

More like this

Matendo ya Polisi ni hujuma dhidi ya utawala bora, demokrasia

MFUMO wa uchumi wa soko huru una kanuni zake. Miongoni mwake ni kuruhusu ushindani....

Lukuvi afariki dunia

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye...

Mgodi wa kihistoria wa niobium kujengwa Mbeya

Na Mwandishi Mbeya TANZANIA imepiga hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na Marekani baada...