WMA yafunga Mtambo wa kisasa unaohakiki Dira za Maji Dodoma

Na Mwandishi Wetu

WAKALA wa Vipimo (WMA) umesimika mtambo wa kisasa wa kidijitali wa kuhakiki dira za maji katika jengo la makao yake makuu lililopo jijini Dodoma.

Meneja Uhakiki wa Vipimo na Viwango wa WMA Makao Makuu, Magesa Biyani amesema usimikaji mtambo huo uliogharimu takribani shilingi milioni 400, utawezesha uidhinishaji na uhakiki wa dira za maji kwa muda mfupi na kwa usahihi zaidi kupitia miradi mingi ya maji inayoendelea kutekelezwa nchini ikiwemo Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine jirani.

Akizungumza na wanahabari wa WMA Februari 3, 2026, Biyani amesema kuwa “Mtambo huu umekuja kwa wakati mwafaka kuwezesha wafanyabiashara pamoja na Mamlaka za Maji kuzingatia kwamba dira za maji zote ambazo wanawafungia wateja katika maeneo yao ziwe zimehakikiwa na WMA ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kulingana na thamani ya fedha wanazolipa.”

Akifafanua zaidi, amesema kuwa mtambo huo una uwezo wa kuhakiki dira za maji nyingi zaidi kwa wakati mmoja kwa kutumia muda mfupi zaidi tofauti na mitambo ya awali ambayo ni ya ki-makenikali (Mechanical Test Bench) yenye uwezo wa kuhakiki dira za maji 10 kwa wakati mmoja ikitumia dakika 20 hadi 30.

Amesema kuwa mtambo huo pamoja na mingine miwili ya aina hiyo iliyoko katika Kituo cha Uhakiki Vipimo, Misugusugu mkoani Pwani, kwa pamoja imeleta faida kubwa ikiwemo kupima dira za maji nyingi zaidi, kwa usahihi zaidi na kwa muda mfupi tofauti na awali kabla ya uwepo wake.

Akitoa mfano, Biyani amesema mathalani kwa Kituo cha Misugusugu ambako mitambo ya aina hiyo ilitangulia kusimikwa kabla ya Dodoma, dira za maji kati ya laki mbili hadi laki tatu zimekuwa zikipimwa kwa mwaka kutegemea na uhitaji kutokana na kuongezeka kwa miradi ya kimkakati.

“Kwahiyo imeleta faida kubwa sana na kusaidia thamani ya fedha iweze kuonekana kwa wateja/wananchi, Mamlaka za Maji na wafanyabiashara na hata kwa uchumi wa nchi,” ameeleza Biyani.

Akidadavua zaidi namna WMA inavyohusika katika uidhinishaji na uhakiki wa dira za maji, ameeleza kuwa hilo ni mojawapo ya majukumu yake ya uhakiki wa vipimo vya aina mbalimbali nchini kwa lengo la kumlinda mlaji.

Amesema kuwa, WMA huidhinisha na kuhakiki vipimo kwa niaba ya Serikali ambapo kwa upande wa dira za maji, mfanyabiashara yeyote binafsi au kampuni kabla ya kuagiza au kuzalisha bidhaa hizo anatakiwa awasilishe sampuli yake WMA ili kuhakiki muundo wake na baada ya kuidhinishwa anatakiwa kuziwasilisha bidhaa zote alizoagiza au kuzalisha ili zihakikiwe kwa kila moja kujiridhisha kuhusu usahihi wake.

Biyani amefafanua zaidi kuwa zoezi hilo hulenga kuzilinda pande zote mbili yaani mteja na muuzaji ili yeyote kati yao asipunjwe.

Dira za maji zilizohakikiwa humuwezesha mteja kulipia kiwango stahiki kulingana na matumizi yake ilhali kwa upande wa muuzaji humwezesha kupata malipo stahiki kulingana na huduma anayotoa.

Akijibu swali la mwandishi kuhusu mipango ya WMA kufikisha huduma hiyo nchi nzima, Biyani ameeleza kuwa Mpango Mkakati wa Wakala wa miaka mitano ijayo kuanzia mwaka huu wa 2026 ni kusimika mitambo ya aina hiyo katika Kanda zote zilizosalia nchini ambazo amezitaja kuwa ni Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Magharibi pamoja na Kanda ya Kusini.

Hata hivyo, ameweka bayana kuwa kutokuwepo kwa mitambo ya kisasa katika Kanda tajwa haimaanishi kuwa kazi hiyo haifanyiki katika maeneo hayo, la hasha, inafanyika kwa kutumia mitambo ya ki-makenikali pamoja na ile midogo inayobebeka (Portable Test Kit) ambayo amesema Maafisa Vipimo kote nchini huibeba mikononi na kwenda nayo katika maeneo mbalimbali kuhakiki dira za maji.

Katika hatua nyingine, Biyani ametoa hamasa kwa wadau wa vipimo mkoani Dodoma na mikoa ya jirani hususani katika sekta ya maji kutumia fursa ya uwepo wa mtambo huo wa kisasa kupeleka dira za maji WMA zikahakikiwe na kuidhinishwa.

Biyani ameonya kwamba ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kufunga na/au kutumia dira ya maji ambayo haijahakikiwa na Wakala wa Vipimo huku akibainisha kuwa adhabu yake huanzia kutozwa faini ya shilingi laki moja hadi milioni 20 kwa kosa la kwanza na shilingi milioni 20 hadi milioni 50 kwa kosa la pili kutegemea na aina ya kosa.

Ametaja gharama za kuhakiki dira za maji kwa mujibu wa sheria kuwa ni shilingi elfu kumi tu kwa kila moja na kwa uidhinishaji wa muundo ni shilingi elfu hamsini.

Sheria ya Vipimo, Sura Namba 340 kupitia kanuni zake mbalimbali inaielekeza WMA kuhakiki dira za maji walau mara moja kila mwaka lakini pia Wakala hufanya kaguzi mbalimbali za kushtukiza ili kubaini endapo kuna udanganyifu na kuchukua hatua.

Wakala imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa vipimo na umma kwa ujumla katika maeneo mbalimbali ikiwemo namna ya kutambua kipimo ambacho kimehakikiwa ambapo kwa upande wa dira za maji, utambuzi kuwa dira husika imehakikiwa ni kwa kuona lakiri iliyofungwa pamoja na muhuri wa WMA ukionesha tarehe, mwezi na muda ambao kifaa hicho kimehakikiwa.

Dira yoyote ambayo haina lakiri na muhuri wa WMA inamaanisha kuwa haijahakikiwa.

spot_img

Latest articles

Benki ya CRDB yaja na ‘Benki Kimpango Wako’ yaahidi huduma bora zaidi mwaka 2026

Na Mwandishi wetu BENKI ya CRDB imezindua kampeni yake ya mwaka 2026 inayoitwa ‘Benki Kimpango...

Serikali kununua matrekta 10,000

Na Mwandishi Wetu WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imepanga kununua matrekta 10,000...

Menejimenti ya TMDA yajipanga na Dira 2050

Na Mwandishi Wetu MENEJIMENTI ya TMDA imekutana Morogoro Februari 2 hadi 3, 2026 kujadili...

Dk. Nchimbi: Uhuru wa Mahakama situmike kuficha uzembe

Na Mwandishi Wetu MAKAMU wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi ametoa rai kwa Majaji na Mahakimu...

More like this

Benki ya CRDB yaja na ‘Benki Kimpango Wako’ yaahidi huduma bora zaidi mwaka 2026

Na Mwandishi wetu BENKI ya CRDB imezindua kampeni yake ya mwaka 2026 inayoitwa ‘Benki Kimpango...

Serikali kununua matrekta 10,000

Na Mwandishi Wetu WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imepanga kununua matrekta 10,000...

Menejimenti ya TMDA yajipanga na Dira 2050

Na Mwandishi Wetu MENEJIMENTI ya TMDA imekutana Morogoro Februari 2 hadi 3, 2026 kujadili...