Na Winfrida Mtoi
WANANCHI Yanga wameichakaza timu ya Mashujaa mabao 6-0, huku nyota mpya wa kikosi hicho Laurindo Aurelio maarufu Depu akitupia bao moja katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo Januari 19,2025 kwenye dimba la KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Depu raia wa Angola ni usajili mpya ndani ya kikosi cha Wananchi ambapo ameonekana kuanza vizuri kwani aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Maxi Nzengeli lakini alifanyikiwa kufunga na kutoa pasi ya bao.
Wachezaji wengine waliofunga katika mchezo huo ni Mohammed Damaro, Duke Abuya, Pacome Zouzoua, Prince Dube na Mudathir Yahya.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 19 na kuongoza msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa imecheza michezo saba ikishinda sita na kutoka sare mmoja, huku Mashujaa ikibaki nafasi ya tano na pointi 13 baada ya michezo 10.
Baada mchezo huo Wanajangwani hao wanajiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambapo wanatarajiwa kukutana na Al Ahly nchini Misri, Ijumaa Januari 23,2025.


