Na Winfrida Mtoi
SHAMRASHAMRA kuelekea Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON-2025), zimezidi kupamba moto, hasa baada ya timu shiriki za michuano hiyo kuanza kuwasili nchini Morocco ambako yatafanyika mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Mashindano hayo yayonatarajiwa kuanza Jumapili Desemba 21, 2025, yakishirikisha mataifa 24, yamekuwa kama fursa ya kipekee kwa baadhi ya nchi za Afrika kuonyesha utajiri wa tamaduni zao kupitia mavazi ya asili.

Kutokana na hilo mashindano hayo yanaonekana si kuhusu mpira pekee bali kuna vionjo vingi vinavyoyamba. Mashabiki wamekuwa wakivutiwa na hali hiyo, kwa mfano ukiangalia jinsi mataifa mbalimbali kama vile Nigeria, Senegal, Mali, Benin na Comoro walivyowasili Morocco ambapo wachezaji wao wameonekana wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni.
Hivyo aina hiyo ya mavazi inaonekana si urembo pekee bali ni utambulisho kimataifa unaoboresha taswira na sifa ya nchi, hali inayosaidia kuvutia watalii.


Afrika Magharibi wameonekana kuwa wazuri zaidi katika ubunifu wa mavazi yao ya kitamaduni tofauti nan chi nyingine kama Tanzania, Zambia, Afrika Kusini, Angola na wengine ambao timu zao zimewasili zikiwa katika mavazi ya kawaida ya kimichezo.
Fainali hizo zinatarajiwa kuanza Jumapili Desemba 21, 2025, jumla ya mataifa 24 yakichuana ikiwamo Tanzania.





