Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeufungia Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mchezo huo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Novemba 26, 2025 na shirikisho hilo, imesema miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.
“Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.
“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” imeeleza taarifa hiyo.
Mechi ya mwisho katika uwanja huo imechezwa leo ya Ligi Kuu Bara ambapo wenyeji Coastal Union imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City.
Uamuzi wa kuufungia uwanja huo umekuja muda mchache baada ya kumalizika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo wenyeji Coastal Union imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City. Timu nyingine inayotumia uwanja huo ni African Sports ya Ligi ya Championship.


