Na Winfrida Mtoi
Jumla ya wanariadha wanawake 155, wanatarajiwa kushiriki katika msimu wa saba wa mashindano ya riadha maarufu ‘Ladies First’ yatakayofanyika kuanzia Novemba 29 hadi 30, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mashindano hayo yanayofanyika kwa ushirikiano wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan( JICA) pamoja na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), yatatanguliwa na semina ya wanariadha na waamuzi Novemba 28, 2025 uwanjani hapo.
Akizungumzia maandalizi ya michuano hiyo leo Novemba 26,2025 mbele ya wanahabari, Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha kila kitu kimekamilika na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi.
Amesema lengo la mashindano hayo ni kuunga mkono jitihada za wanawake katika michezo huo yakihusisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tunafahamu kuwa ushiriki wa wanawake katika michezo bado uko chini ukilinganisha na wanaume, licha ya juhudi za Serikali na wadau mbalimbali kupambana na hali hiyo,” amesema Neema.
Amesema wanariadha hao watashindana katika mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1500, 5000,4*100 kupokezana vijiti( Relay) pamoja na kurusha mkuki.
Aidha ameeleza mafunzo yatakayotolewa wakati wa mashindano ni pamoja na matumizi bora ya taulo za kike, nidhamu ya ya fedha na upimaji wa afya kwa washiriki.
Katika hatua nyingine Katibu huyo amemshukuru Kanali Mstaafu na Mwanariadha mkongwe Jumaa Ikangaa kwa kuamua kuanzisha mashindano hayo akishirikiana na Serikali ya Japani kupitia JICA.
Ametoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji na kutoa hamasa kwa wanariadha wa kike wanaokuza mchezo wa riadha nchini.
Naye Rais wa RT, Rogath Stephen amesema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa Taifa kutokana na kuongezeka idadi ya wanariadha wa kike tofauti na miaka ya nyuma.
“Kupitia mashindano haya tumeweza kupata wanariadha wengi wa kike ambao wamefanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa nje ya nchi na kuipeperusha vema bendera ya Taifa letu,” amesema.
Kwa upande wake muasisi wa Ladies First, mwanariadha mkongwe Kanali Mstaafu Ikangaa amesema wanariadha wote waliofanya vizuri wamepitia mashindano hayo,hiyo kuiongeza BMT kutokana na juhudi inayofanya katika kuibua vipaji vya watoto wa kike.


