Na Winfrida Mtoi, The Media Brains
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umekiri kuwa vita ya kudhibiti jezi feki ni ngumu pamoja na jitihada wanazofanya na kutumia mbinu nyingi lakini imeshindikana, walichofanikiwa ni kupunguza madhara na si kukomesha suala hilo.
Hayo yamezungumzwa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe leo Septemba 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa jezi mpya toleo la pili ya timu hiyo.
“Vita ya jezi feki sio vita nyepesi, ni vita ngumu mmno, ni vita nzito kupambana nayo, tumetumia mbinu nyingi, tulichofanikiwa ni kupunguza madhara lakini hatujafanikiwa kukomesha tatizo hilo.

“Sisi tumezindua jezi hivi karibuni na mzigo wetu tulioleta msimu huu umeisha, lakini cha ajabu bado tunaendelea kupewa taarifa kuwa mizigo mikubwa ya jezi bado inaendelea kuingia nchini. Ila uongozi wa Yanga umekuja mpango wa kukomesha hili mwaka huu. Naamini njia tuliyokuja nayo hii itakuwa ni komesha,” amesema Kamwe.
Ameeleza kuwa wamedhamiria kupambana na hata toleo hilo jipya ni moja ya suluhisho kwa kuwa hawawezi kuona klabu inazidi kupoteza mapato na kuwanufaisha wengine.
Hivi karibuni uongozi wa Klabu ya Simba nao ulitoa taarifa za uwepo wa jezi feki zinazouzwa katika mikoa mbalimbali kama vile Morogoro, Singida, Geita na Mwanza.
Mwaka 2023 Ofisa Habari wa Yanga, Kamwe aliongoza zoezi la kukamata jezi feki za Yanga na Simba kwenye godauni moja maeneo ya Mbozi Road, Temeke, Dar Es Salaam zilizokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya sh. 10 bilioni.