Na Winfrida Mtoi
Bingwa wa Dunia wa mbio za Marathoni za kilomita 42, ambaye ni Askari wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), Sajenti Alphonce Simbu, amesema si rahisi kushinda lakini ukijiandaa, kujituma na kufanya juhudi, unafanikiwa.
Simbu ambaye ameshinda medali ya dhahabu katika mashindano yaliyofanyika Tokyo, nchini Japan, amewaslli leo saa 9:13 alfajiri na kupokelewa na watu mbalimbali pamoja na familia yake.

Akizungumza baada ya kuwasili amewataka wanamichezo wa kitanzania hasa riadha, kufanya juhudi na kujiandaa na wasikate tamaa katika kufikia ndoto zao.
“Niwasihi tu wachezaji wa kitanzania kwamba wanaweza na wasikate tamaa kwa sababu ukikata tamaa unaweza usifikie ndoto zako. Niwaambie tu juhudi, kujituma na nidhamu zinasaidia,” amesema Simbu.
Simbu aliibuka mshindi akitumia muda wa 2:09:48, akiwashinda wanariadha 89 kutoka nchi mbalimbali.