Na Winfrida Mtoi
Chama Cha ACT Wazalendo kimegoma kupokea gari la Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kikidai kuwa kinazo rasilimali za kutosha za kuwawezesha kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kampeni.
Hayo yamejitokeza leo Septemba 13, 2025 wakati Mgombea wa Urais wa ACT, Luhaga Mpina na Mgombea Mwenza wake, Fatma Abdulhabib Ferej waliporejesha fomu ya uteuzi katika Ofisi Ndogo za INEC, jijini Dar es Salaam.
Msimamo wa ACT Wazalendo wa kukataa gari hilo umetolewa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho mbele ya Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele.

Naye Mgombea Urais wa ACT, Mpina amesisitiza kuwa huo ndio msimamo wa chama hizo na mgombea mwenza kwa sababu haina haja kuchukua gari hiyo wakati wanazo rasilimali za kutosha.
“Kwa nini tuchukue gari ambalo linaweza kutumika na watanzania kwa matumizi mengine. Kuhusu suala la kupewa mlimzi hilo tumekubaliana nalo kwa sababu lipo kisheria,” amesema Mpina.
Ameeleza kuwa licha ya kuchelewa kuamza kampeni, wanaami siku zilizobaki zitawatosha kabisa kuwafikia watanzania wote kunadi sera zao, huku akijinasibu kuwa atapata ushindi wa asilimia 70 na asilimia 30 watakawana wagombea wengine.
“Hizi siku 45 sisi zinatutosha na tutatembea majimbo yote. Tutazindua kampeni zetu mapema tu kila kitu kitakaa sawa kwa wakati,” amesema.
INEC imeweka utaratibu wa kutoa gari na dereva kwa kila mgombea wa Urais wa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa 2025.