Na Winfrida Mtoi
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imemteua rasmi Luhaga Mpina kuwa Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha ACT Wazalendo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Mpina ameteuliwa pamoja na mgombea mwenza wake, Fatma Abdulhabib Ferej, ambapo leo Septemba 13, 2025 walifika katika Ofisi Ndogo za INEC na kukabidhiwa fomu ya uteuzi na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele.
Katika tukio hilo, Mpina aliambatana na viongozi mbalimbali waandamizi wa chama hicho pamoja na wafuasi waliokuwa wakishangilia hatua ya chama chao kufanikisha uteuzi huo.


Akizungumzia uteuzi huo, Mpina amesema hatua ya INEC kuwateua rasmi inaashiria kuwa safu yao imekamilika na watashirikiana kuhakikisha wanatumia siku za kampeni zilizobaki kufikia majimbo yote ya Tanzania.
Mpina amerejesha fomu ikiwa ni siku mbili baada ya kushinda kesi ya kupinga kuenguliwa kwenye mchakato wa uteuzi wa wagombea.