Na Mwandishi Wetu
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesitisha mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), uliopangwa kufanyika Oktoba 4, 2025 baada ya kubainika kutumia Katiba isiyo halali.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo leo Septemba 9,2025, imetaja sababu ya kusitishwa kwa mchakato wa uchaguzi huo ni kutokana na kukiukwa kwa taratibu, hivyo kutakiwa kuanza upya.
Taarifa hiyo imesema uamuzi huo wa kusitisha mchakato wa uchaguzi umetolewa na Waziri Pro. Palamagamba Kabudi, akiitaka TOC kuanza upya kwa kutumia Katiba inayotambulika na kisheria na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), iliyoidhinishwa Novemba 26, 2020.
“Wizara imechukua hatua hiyo kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, uwajibikaji, utawala bora na utulivu katika sekta ya michezo,” imesema.
Aidha, Wizara imesisitiza kuwa rufaa iliyowasilishwa na uongozi wa TOC kuhusu zuio la awali la Msajili wa Vyama vya Michezo, ilikataliwa, na hivyo ni lazima kufuata maelekezo ya Serikali.


