Na Mwandishi Wetu
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeandika historia kwa mara kwanza kwa kutinga robo fainali ya michuano ya CHAN ikiichapa Madagascar mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa leo Agosti 9, 2025 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Stars iliyopo kundi B imefikisha pointi tisa, huku ikiwa imebakiwa na mechi moja dhidi ya Afrika ya Kati ambayo inaburuza mkia katika kundi hilo.
Taifa Stars imekuwa timu ya kwanza kutinga robo fainali katika michuano hiyo ikiwa haijapoteza mechi hata moja katika tatu ilizocheza.

Ilianza mechi ya ufunguzi ya michuano hiyo kwa kuitandika Burkina Faso mabao 2-0, ikaichapa Mauritania bao 1-0 na leo kuikung’uta Madagascar 2-1, mechi zote zikipigwa dimba la Mkapa.
Ukiangalia msimamo ulivyo katika kundi B, Burkina Faso pekew ndiyo ina uwezo wa kufikisha kufikia alama tisa kutokana na kucheza mechi mbili na kupata pointi tatu, imebakiza michezo miwili.
Nafasi ya pili ipo Mauritania na pointi nne ikicheza mechi tatu, namba tatu ni Madagascar yenye alama moja na imecheza michezo miwili, mwisho yupo Afrika ya Kati aliyecheza mechi tatu bila kupata pointi yoyote.