Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa SELF MF umewakaribisha wananchi kutembelea Banda lao lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu ya kifedha, mikopo yenye masharti nafuu, pamoja na huduma ya bima ya mazao.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) kitaifa yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja Masoko na Uhamasishaji wa SELF MF, Linda Mshana, amesema wananchi wana nafasi ya kipekee kufika kwenye mabanda ya SELF na kujifunza namna ya kujiimarisha kiuchumi kupitia huduma za kifedha, hususan mikopo kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wa nishati mbadala.

“Tunaendelea kuwahamasisha Watanzania, hasa vijana, kutumia fursa hizi. Mikopo yetu inaangalia msimu wa shughuli zako iwe ni kilimo, ufugaji au biashara. Hii inasaidia kuhakikisha marejesho hayakusumbui. Unarejesha kwa utaratibu kulingana na muda unaofaa,” amesema Mshana.
Amesisitiza kuwa, vijana wanayo nafasi kubwa katika kukuza uchumi kupitia kilimo cha kisasa, na kuwataka kuchukua hatua ya kuomba mikopo kwa ajili ya kuwekeza kwenye umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, na mbolea ili kuongeza tija.
Katika maonesho hayo, SELF imewasilisha pia mfano wa mafanikio ya mteja wao, kijana Faustine Masanja, ambaye aliweza kuanzisha mradi wake unaoitwa Kahawa Mkononi kupitia mkopo alioupata kutoka SELF MF kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo (kupitia mpango wa BBT) na Bodi ya Kahawa Tanzania.

Akisimulia safari yake, Masanja amesema: “Tulikutanishwa na SELF baada ya kupata mafunzo ya biashara kutoka Wizara ya Kilimo na Bodi ya Kahawa. Leo hii, biashara yetu ya kahawa ya kisasa imekuwa msaada mkubwa kwa vijana. Tunauza kahawa mitaani kwa njia za kisasa na hii imewasaidia vijana kujitegemea kiuchumi,”.
Masanja ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Bodi ya Kahawa na SELF MF kwa kushirikiana kufanikisha mradi huo wa vijana, na kuwasihi vijana wengine wasibaki nyuma.
“Fursa zipo, na zinaweza kubadili maisha yako. Kinachotakiwa ni uthubutu, nidhamu na kujitokeza pale panapotolewa nafasi kama hizi,” ameongeza.
SELF Microfinance, ambayo ipo chini ya Wizara ya Fedha, imejikita katika kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa Watanzania wa kada mbalimbali wakiwemo wafanyakazi wa taasisi za umma, asasi za kifedha zinazotoa huduma za mikopo, pamoja na wakulima na wafanyabiashara wadogo.
SELF Microfinance imedhamiria kuendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kutoa mikopo bunifu, elimu ya fedha, na kusaidia wananchi hasa wa kipato cha chini kuinuka kiuchumi kupitia sekta muhimu kama kilimo, uvuvi, ufugaji na Nishati Mbadala.