Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Nyangassa, amepongeza juhudi zinazofanywa na Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) katika kuhamasisha kilimo cha mkonge, ambazo zimewezesha kupatikana kwa zaidi ya wakulima 15 wenye jumla ya ekari 240 ndani ya muda mfupi.
Akizungumza leo Jumatano mara baada ya kutembelea banda la TSB katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Fatma amesema ameridhishwa na hatua hiyo, huku akionesha nia ya kuona Mkoa wa Dodoma, hususan Wilaya ya Kondoa, inakuwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo.

“Nimefurahishwa sana na kazi nzuri mnayofanya, na matarajio yangu ni kuona Wilaya ya Kondoa inaongoza kwa uzalishaji wa mkonge,” amesema Fatma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka TSB, Simon Kibasa, amesema Mkoa wa Dodoma bado uko kwenye hatua za awali za kilimo cha mkonge kutokana na wakulima wengi kuwa katika maandalizi au wameshapanda lakini hawajaanza kuvuna.

“Uzalishaji wa mkonge nchini umeongezeka kutoka tani 39,484 mwaka 2021 hadi kufikia tani 61,215 kwa sasa. Mkoa wa Tanga unaongoza kwa uzalishaji kwa takribani tani 34,000,” amesema Kibasa.
Ameongeza kuwa hamasa ya serikali na Bodi imechangia ongezeko la wakulima wapya katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Dodoma.

“Kwa sasa kuna zaidi ya ekari 240 zinazolimwa mkonge Dodoma kutoka kwa wakulima waliotembelewa, na tunaamini zitaongezeka kwani bado kuna wakulima ambao hatujawafikia,” amesema.
Kibasa ameeleza kuwa kupitia maonesho hayo, wakulima watatu kutoka Dodoma wamejitokeza na kuomba kutembelewa kwa ajili ya usajili na bodi, na kwamba watafikiwa mara baada ya maonesho kumalizika.


