Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limepokea taarifa za kuchukuliwa na watu asiowafahamu na kurejeshwa kwa mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Christina Polepole, mwenye umri wa miaka 52, mkazi wa Bahari Beach, mtaa wa Katumba, Kinondoni.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Julai 18,2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro tukio hilo lilianza kuripotiwa kupitia mitandao ya kijamii mnamo Julai 17, 2025, ambapo mtu aliyejitambulisha kwa jina la Humphrey Polepole akijieleza kuwa dada yake alichukuliwa na watu wasiojulikana waliovamia nyumba yake kwa kuruka ukuta.
“Dada huyo alifika mwenyewe katika kituo cha Polisi Kawe na kutoa taarifa kuwa jana alichukuliwa na watu ambao hakuwafahamu na baadae walimrudisha nyumbani kwake jana hiyo hiyo,” ameeleza Muliro.
Jeshi hilo limethibitisha kuwa linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kwa kushirikiana na wananchi pamoja na vyombo vingine vya usalama, huku likitoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati taratibu za uchunguzi zikiendelea.
Aidha Kamanda Muliro amesema kwa kushirikiana na wananchi Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha usalama katika jiji la Dar es Salaam.