Na Winfrida Mtoi
Wachezaji wa Yanga, Kibwana Shomari na Denis Nkane wamajitosa kwenye mchezo wa ngumi ambapo Julai 26, 2025 wanatarajiwa kupanda ulingoni kuzichapa katika pambano la utangulizi kwenye usiku wa Dar Boxing Derby, viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.
Katika kujiandaa na mchezo huo, Kibwana anajifua kwenye kambi ya bondia Twaha Kiduku Morogoro, huku Nkane akifanya mazoezi kambi ya Naccoz chini ya Mfaume Mfaume.
Mabondia hao wapya mjini wametambuliwa leo Julai 15, 2025 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na uongozi wa Peaktime Media ambao ndiyo waandaaji wa Dar Boxing Derby.

Baada ya utambulisho huo, wachezaji hao walipewa nafasi ya kila mmoja kuelezea alivyojindaa kumkabili mwenzake ambapo walitoleana maneno makali yaliyosabisha watake kupigana mbele wanahabari.
Alianza kutamba Kibwana anayewakilisha Morogoro na kusema Nkane amekuwa akimzoea siku nyingi hivyo amepata nafasi ya kumaliza hasira zake kwa kumpa kipigo ambacho hatasahau maishani mwake.
“Huyu kijana mdogo amekuwa akiniposti vibaya mitandaoni, nimekua nikimuangalia tu, huu ni wakati kumfundisha adabu na nitampiga na ngumi inaitwa ‘kata funua,” ametamba Kibwana.

Naye Nkane akashindwa kuvumilia alianza majigambo yake kwa kejeli akimuita Kibwana ni babu mwenye kipara na anakwenda kumuongezea kitu kingine kwa kumpiga hadi meno yatoke ili abaki na mapengo.
“Naomba kama sheria inaruhusu tuanze kupigana hapa hapa, nataka nimkaribishe vizuri Dar es Salaam maana kipindi kile alikuja alishukia Ubungo na mabegi yake. Ngumi ninayokwenda kumpiga nayo inaitwa jiwe na si jiwe yaani lina madini ndani yake,” amejinadi Nkane.
Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema uongozi umewapa baraka zote wachezaji hao, lengo likiwa ni kuendeleza vipaji vya michezo mingine na si mpira wa miguu pekee.

” Sisi tunaitwa Young Africans Sports Club na ukingalia nembo yetu pale kuna picha mcheza ngumi, hivyo kupitia pambano hili tunakwenda kufahamu yule bondia pale kwenye nembo yetu ni nani,” amesema Kamwe.
Aidha Promota wa pambano hilo, Seleman Semunyu, ameeleza kuwa katika mapambano yote 11 yanayokwenda kupigwa siku hiyo, amefuatilia maandalizi na mabondia wote wapo vizuri kiafya hadi sasa.
Pia ameushukuru uongozi wa Yanga kwa ushirikiano wanaoonesha kila wanapowapelekea wazo pamoja na kuwaruhusu wachezaji hao.
“Nawashukuru Yanga kwa kuridhia wazo hili. Tunaamini mashabiki na wanachama wa Yanga watatuunga mkono.Tuna wadhamini Euromax wameanza kutuunga mkono kwenye hili, tunawahamasisha na wadhamini wengine waendelee kujitokeza,” amesema Semunyu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Euromax,, Peter Michael, amesema wamefurahishwa na mchango wa Peak Time katika kukuza mchezo wa ngumi nchini na kwamba anaamini pambano litakuwa la kuvutia na wao watakuwa sehemu ya maendeleo haya ya michezo.