Na Tatu Mohamed
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema kuwa hadi kufikia Juni 30, 2025, tayari Sheria 300 kati ya 446 zimetafsiriwa kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), ikiwa ni juhudi za serikali kuhakikisha Watanzania wanaelewa sheria zinazowaongoza.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la OCPD katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dk. Ndumbaro alisema serikali imetenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kutafsiri sheria 146 zilizobaki.
“Ni muhimu Watanzania waweze kuelewa sheria kwa lugha wanayoitumia kila siku. Hii ndiyo maana tunasisitiza tafsiri ya sheria kwa Kiswahili,” alisema.

Alibainisha kuwa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria ni kiungo muhimu katika mchakato mzima wa utungaji, marekebisho na ufasili wa sheria kabla hazijawasilishwa bungeni.
“Bila ofisi hii, hakuna sheria inayotungwa au kufanyiwa marekebisho. Iwapo sheria zitakuwa na makosa, hata mahakama inaweza kutoa maamuzi yasiyo sahihi,” aliongeza.
Aidha, Dk. Ndumbaro alisema hatua ya kutafsiri sheria kwa Kiswahili inalenga kuwasaidia wananchi wa kawaida, wakiwemo wanafunzi na wanasheria, kuelewa vyema misingi ya sheria nchini.