Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kudhihirisha uwezo wake kama nguzo ya mawasiliano ya kisasa nchini, kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo, TTCL limejipambanua kama muunganishaji thabiti na wa kuaminika, likijikita zaidi katika kutoa huduma salama, bunifu na zenye kuakisi mahitaji halisi ya taasisi za umma, binafsi pamoja na wananchi.
Akizungumza katika banda la TTCL namba 26, Meneja wa Banda hilo, Bi. Janeth Maeda, amesema shirika hilo lipo kwenye maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu mchango wake katika TEHAMA na namna linavyotekeleza wajibu wake kama mtoa huduma wa kimkakati aliyeaminiwa na serikali.

“TTCL ni suluhisho la sasa na baadaye katika sekta ya mawasiliano. Serikali imetuamini kusimamia miundombinu muhimu kama Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC),” alisema Bi. Maeda.
Ameongeza kuwa TTCL inahudumia taasisi mbalimbali za serikali, sekta binafsi na zisizo za kiserikali zikiwemo taasisi za fedha, wizara, mashirika ya umma, sekta ya madini, afya, elimu, usafirishaji na utalii.
Huduma hizo zimekuwa chachu ya mafanikio kwa taasisi hizo kwa kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kuimarisha usalama wa taarifa.
“Teknolojia yetu ya fiber optic imewezesha mashirika haya kufanikisha kazi zao kwa kasi na usalama wa hali ya juu, tukichangia katika maendeleo endelevu ya taifa,” alisisitiza.

Aidha, Bi. Maeda ametoa wito kwa Watanzania, wadau wa biashara, wageni kutoka mataifa mbalimbali, kampuni na mashirika mbalimbali kutembelea banda la TTCL ili kujionea teknolojia ya kisasa ya mawasiliano, kujifunza mbinu za kidijitali za kuhifadhi taarifa salama na namna ya kuongeza tija kwenye shughuli zao kwa gharama nafuu.
Katika msimu huu wa sabasaba, TTCL pia imepunguza bei ya vifaa vya mobile kama Router, USB modem na MiFi, ili kuwawezesha wateja wake kuunganishwa na ulimwengu wa kidijitali kwa urahisi zaidi.
Maonesho hayo yanatarajiwa kuendelea hadi Julai 13, 2025, ambapo TTCL itaendelea kutoa elimu na huduma kwa wananchi.