Na Mwandishi Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Msumbiji katika kuleta maendeleo , ustawi wa wananchi ikiwamo kuimarisha uhusiano kibiasharana baina ya nchi hizo mbili na kukuza mshikamano barani Afrika
Akihutubia katika Sherehe za Madhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Msumbiji leo Juni 25,2025 kwenye Uwanja wa Machava jijini Maputo, Rais Samia amesema uhusiano wa Tanzania na Msumbiji si majirani tu bali ni ndugu wa damu na uliimarishwa zaidi na Waasisi wa Mataifa hayo mawili.
Ameeleza kuwa katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara, Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL), linatarajia kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Msumbiji mwaka huu.

“Katika kuzidi kufungua fursa zaidi za biashara baina ya wananachi wa Msumbiji na Tanzania, ninayo furaha kueleza kuwa, Shirika la Ndege la Tanzania linatarajia kuanza safari za ndege kati ya Tanzania na Msumbiji mwisho wa mwaka huu, hatua itakayoimarisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya watu wetu”, amesema Rais Samia.
Amesema Bara la Afrika imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika hatua ya kwanza ya ukombozi, yaani uhuru wa kisiasa, hivyo kama viongozi wanapaswa kuhakikisha nchi zinakuwa na amani na umoja wa kitaifa ili kuweza kushirikiana kufanikisha hatua nyingine za mageuzi ya kifikra, na kutafuta uhuru wa kiuchumi.

Rais Samia amesema katika kufikia hatua hiyo ni njia mojawapo ni kuhakikisha watu wanaunganishwa pamoja na kuleta Umoja wa Kitaifa, hivyo anaamini chini ya uongozi wa Rais Daniel Chapo wa Msumbiji wataendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Leo tunaposhuhudia ndugu zetu wa Msumbiji wakisherehekea Miaka 50 ya Uhuru wao, nasi ndugu zenu Watanzania tunashereheka pia. Ushindi wa Msumbiji ni ushindi wetu, mafanikio ya Msumbiji ni mafanikio yetu pia, na maendeleo ya Msumbiji ni maendeleo yetu sote,” ameeleza Rais Samia.


Aidha amepongeza hatua ya maendeleo iliyofikiwa na Msumbiji katika kipindi cha miaka 50, hasa nyanja za elimu afya na miundombinu ambayo yaliletwa na dhamira ya kujenga jamii jumuishi na yenye matumaini.
Akizungumzia historia ya Uhuru wa nchi hiyo, Rais Samia amesema Tanzania ilikuwa na mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa Msumbiji kwa kuwapa hifadhi, licha ya kukabiliwa na changamoto za kiuchumi na matishio kutoka kwa waliokuwa wakoloni.

“Tulikuwa tayari kuchelewesha maendeleo yetu ili kuhakikisha ndoto ya ukombozi Msumbiji na mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika inatimia,” amesema.
Katika hatua nyingine Rais Samia ametembelea eneo la kumbukumbu ya Mashujaa wa Msumbiji, jijini Maputo na kuweka shada la maua kama ishara ya heshima kwa Mashujaa waliopoteza maisha wakipigania Uhuru wa nchi hiyo.