Na Mwandishi Wetu
Watumishi wa Umma wameaswa kuendelea kuzingatia miiko na maadili ya utumishi wa umma, sera za nchi, sheria, kanuni na miongozo iliyopo ambayo inahitaji ukarimu, kuwapokea, kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi ipasavyo.
Maelekezo hayo yametolewa leo Juni 23,2025 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akihitimisha kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na Uzinduzi wa Mifumo ya Kidijiti kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Majaliwa amesema ni vyema kuimarisha mikakati ya kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kutumia fursa za uwepo wa maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ili wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata huduma zinazotolewa na Serikali kwa haraka zaidi.

Wakati akizindua mfumo huo amezitaka Taasisi zote za umma kutekeleza agizo la Rais Samia la kuhakikisha kuwa taasisi zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo inayosomana na zinaweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo ili kuboresha huduma ndani ya Serikali.
“Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA hakikisheni kwamba mifumo iliyounganishwa inendelea na majukumu yake ya kubadilishana taarifa lakini pia kila anaeingia mjiridhishe kuwa ana uwezo wa kuwasiliana na yeyote alioko kwenye mfumo, amesema Majaliwa.
Vile vile Mhe. Majaliwa aliwaasa watumishi wa umma kote nchini kujisajili katika mfumo wa kidijitali wa e – wezesha, ambao unawezesha watumishi wa umma kuwekeza moja kwa moja kupitia makato ya mshahara au mapato mbalimbali ya biashara.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, ambayo yalianza tarehe 16 Juni, 2025 na kuhitimishwa leo tarehe 23 Juni, 2025 yameshirikisha Taasisi za Serikali 146, ikiwemo Wizara ya Fedha, pamoja na wafanyabiashara wa makundi mbalimbali.