Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ukaguzi wa viwanja vitakavyotumika kufanyia mazoezi kwa timu zitakazo shiriki michuano ya CHAN Agosti 2025 na AFCON 2027 kwa ushirikiano na nchi za Kenya na Uganda na kuagiza ukamilishwaji wa ukarabati haraka.
Akizungumza jana Juni 16, 2025 baada ya ukaguzi wa viwanja vya Gymkhana, Meja Generali Isamuhyo na kiwanja cha Chuo cha Sheria (Law School ), Majaliwa ameitaka kamati inayosimamia ujenzi huo kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.

“Ni lazima tuwajibike kila mmoja na hasa wale ambao tumepewa majukumu, suala la AFCON na CHAN halina mjadala, tunataka michezo hii ichezwe hapa, tukishindwa watanzania hasa wapenda michezo hawatatuelewa, kila mmoja aone ana nafasi muhimu kufanya kazi hii,” amesema.

Pia Majaliwa ameiagiza kamati hiyo kuhakikisha inasimamia ubora wa ujenzi wa kila eneo kwani hata baada ya michezo hiyo nchi itabaki na miundombinu ya viwanja ambavyo vipo kwenye ubora mkubwa.
Aidha, Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya ReformSports inayotekeleza ukarabati wa eneo la kuchezea la viwanja hivyo kwa kuendelea kusimamia ubora “Mnafanya kazi nzuri sana, tunawashukuru sana”