Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka ili kujenga kanda salama na wenye maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Ameyasema halo leo Juni 6,2025 wakati akifunga Mkutano wa 30 wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia Shirikisho la Wakuu wa Polisi wa nchi wanachama wa SARPCCO katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi wanachama kuhakikisha utekelezaji wa mikakati hiyo kwa vitendo.
Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camillus Wambura, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa SARPCCO amesema mkutano huo umejikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
IGP Wambura ameongeza kuwa Mkutano huo umejadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za uhalifu ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa, kuimarisha uwezo wa kiufundi na kuanzisha operesheni za pamoja.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Sekretarieti ya SADC, Profesa Kula Theletsane, amehimiza umuhimu wa ushirikiano wa kanda katika kukabiliana na uhalifu wa kimataifa unaovuka mipaka.
Amesema wamekubaliana kwa kauli moja kuimarisha ushirikiano wao katika kukabiliana na uhalifu huo na wamejizatiti kuanzisha mikakati ya pamoja itakayowezesha kubadilishana taarifa za kijasusi, kuimarisha mawasiliano kati ya nchi wanachama na kuanzisha operesheni za pamoja.