Na Mwandishi Wetu, Media Brains
Mwandishi wa Habari Mkongwe, Absalom Kibanda ambaye pia ni Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni ya Media Brains, amezawadiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutokana na mchango wake katika tasnia ya habari nchini.
Zawadi hiyo ya fedha taslimu Sh 10 milioni, imekabidhiwa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa utoaji tuzo za Samia Kalamu Awards 2025, jijini Dar es Salaam.

Kibanda amepewa zawadi hiyo pamoja na wakongwe wengine ambao ni Deodatus Balile, Haula Shamte na Baraka Islam kutokana na uandishi wao mahiri wa habari na uchambuzi hasa katika masuala ya siasa.
Akizungumza wakati wa kutoa zawadi hizo, Prof. Kabudi amesema habari na makala ambazo wameziandika wakongwe hao zimekuwa mchango mkubwa na zimewaleta watanzania pamoja bila kuligawa Taifa.

“Mheshimiwa Rais nawiwa wingi wa shukrani kwa waandishi wenzangu wa habari, na wapo waandishi wa habari mahiri wa habari za siasa zenye uchambuzi wa kina, zinazojenga umoja, uzalendo, mshikamano na zinazotambua hatua kubwa za kimaendeleo ambayo Taifa letu limepga hasa katika miaka hii minne ya uongozi wako.
“Habari na makala ambazo wameziandika Mheshimiwa Rais ni makala ambazo zimetuleta pamoja, zimetujenga pamoja na ni makala ambazo haziligawi Taifa. Kawa kutambua mchango wa hao waandishi wa habari, Wizara imeona ni vyema nao watunukiwe zawadi na wizara,” ameeleza Prof. Kabudi.