Ni sabuni gani itamtakatisha Mkapa?

WIKI iliyopita katika safu hii niliuliza wako wapi watetezi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, wajibu hoja mbalimbali za kukengeuka kimaadili kwa kiongozi huyu aliyeingia madarakani akionekana kama kiongozi mwadilifu na msafi hadi akapewa jina la Mr. Clean.

Kwa bahati nzuri, serikali imeamua kubeba wajibu huo, si kwa mara ya kwanza; kwani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipata kutamka bungeni kwamba Mkapa ni mtu safi, na aliwapa changamoto wanaomchafua Mkapa wasema kama kiongozi huyo ana akaunti ya fedha ughaibuni, au kama ana shirika la ndege lililoandikishwa kwa jina lake? Pinda alikuwa akieleza kwamba kiongozi huyo anaandamwa bure!

Wiki iliyopita kwa bahati nzuri kile ambacho serikali ilikuwa ikiwaza, yaani kuutwaa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, kiliwekwa wazi. Lakini katika kuweka wazi, juhudi ile ile ya kutaka kumtakatisha Mkapa ilionekana wazi.

Wizara ya Nishati na Madini iliweka wazi kwamba eti wakati kampuni ya Tan-Power Resources inasajiliwa ikiwa ni mjumuiko wa makampuni manne, ANBEM ambayo ni mali ya Rais Mkapa na mkewe, Anna, ingawa ilikuwa imeonyesha nia ya kununua hisa kwenye kampuni hiyo, lakini haikuwa imetoa fedha zozote kwa maana hiyo wakati wa kusajiliwa ni wazi ANBEM haikuwa mwanahisa wa Tan-Powers Resource Limited.

Kwa maana hiyo, Rais Mkapa hawezi kutajwa kwamba ni mmoja wa wamiliki wa Tan-Power Resources Limited na kwa maana hiyo si mmoja wa wamiliki wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.

Kwa hali hii na kwa fikra za walioko serikalini Mkapa amesafishika!

Huko nyuma niliwahi kuandika kwamba kuna watu wanaoitwa spin doctors hawa ni watalaam wa mawasiliano, wenye ujuzi wa kusuka maneno ili kuwasilisha ujumbe unaoonyesha sura nzuri ya serikali kwa wananchi wakati wote.

Wataalam hawa wanaweza kuufanya umma usadiki mchana ni usiku na kinyume chake. Kama kuna kiongozi duniani aliyewahi kutumia ma-spin doctor mpaka akaingia madarakani na kuonekana ni mmoja wa viongozi shupavu wa karne hii, ni aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.

Huyu kwa nguvu za ma-spin doctor wake aliisadikisha dunia kwamba Saddam Hussein, rais wa zamani wa Iraq alikuwa ni mtu hatari na mwenye silaha za maangamizi kiasi kwamba kama asingedhibitiwa mara moja dunia ilikuwa hatarini.

Dunia inafahamu uongo huu wa ma-spin doctor wa Blair haukufika mbali sana, kwani baada tu ya kuanza kwa vita ya Iraq ya mwaka 2003, hakuna silaha yoyote ya maanagamizi makubwa iliyokutwa, lakini Saddam hakuwa tena madarakani. Kwa maana hiyo nia yao ya kumuondoa Saddam ilitimia hata kama hakukuwa na ushahidi wa makosa yake.

Sasa tukirejea hapa kwetu, wataalam ndani ya serikali, hususan ndani ya Wizara ya Nishati na Madini, wametoa utetezi wa Mkapa. Utetezi wenyewe ni mwepesi mno, ni wazi kwamba kama taarifa hiyo iliandaliwa na ma-spin doctor ni lazima warudi darasani kwa kujifunza vizuri zaidi jinsi ya kusuka maneno ili ujumbe wao ufike vilivyo.

Utetezi wa serikali kwa Mkapa ni sawa kabisa na mtu mwovu mwenye nia mbaya alivunja nyumba ya mtu hadi kuingia ndani, lakini hakuiba chochote kwa sababu ama mwenye nyumba alishtuka au hali ya hewa ilibadilika na akakimbia kabla ya kuiba. Lakini la kushangaza mtu huyo anajitapa kwamba hana kosa kwa sababu eti hakuiba.

Kinachosumbua hapa ni nia ovu! Na kwa Mkapa kinachosumbua hapa hata kama leo hana hisa ndani ya Tan-Power Resources ni nia ovu! Mkapa hakuacha kulipa hisa zake ndani ya Tan-Power Resources kwa sababu aligundua kwamba kampuni hii ilikuwa na nia ovu ya kumilikishwa mgodi wa umma bila kuwepo ushindani wa zabuni.

Kama Mkapa angegundua kuwepo kwa nia ovu, yaani uvunjaji wa taratibu na kanuni tena viongozi wenye dhamana na mgodi huo wakiwa wamejipanga kuununua kwa bei ya kutupa, si tu asingelipia hisa za Tan-Power Resources, bali hata mwanaye asingelipia hisa zake kwenye kampuni hiyo hiyo.

Kwa faida ya wasomaji wa safu hii niwakumbushe tu wamiliki wa Tan-Power Resources Limited ni pamoja na kampuni ya Fosnlid ambayo wamiliki wake ni Nick Mkapa, Fostar Mkapa na B. Mahembe wakati kampuni ya Devconsult LTD wamiliki wake ni D.Yona na Danny Yonna J.R.

Pia kuna kampuni za Choice Industries ambayo wamiliki wake ni Joe Mbuna na Goodyeer Francis na kampuni nyingine ni Universal Technologies ambayo inamilikiwa na Willfred Malekia na Evance Mapunda.

Kwa akili ya kawaida tu utaona wazi kwamba Mkapa anaonekana ndani ya Tan-Power Resources ama kupitia kwa wanaye wawili, Nick na Foster, au kwa waziri wake aliyekuwa na dhamana na madini wakati huo, Daniel Yona ambaye yumo dhahiri kupitia Devconsult LTD akiwamo yeye na mwanaye, Junior Yona.

Kwa hali yoyote ile shughuli ya Tan-Power Resource iliyoanzishwa Julai 2005, yaani wakati nchi imezama kwenye harakati za uchaguzi, ilikuwa ni kuwezesha watu fulani kutwaa Kiwira. Na utwaaji wenyewe hakuwa wazi. Mpaka leo ma-spin doctor ndani ya serikali na hata wa kukodisha hawajaweza kueleza ni kwa njia ipi makampuni haya ambayo wamiliki wake wana uhusiano na Mkapa wa kifamilia au kiutendaji serikalini walijua je kuwepo kwa mchakato wa kuuza Kiwira?

Kwa maana hiyo, uundaji wa Tan-Powers Resources na hatimaye kuelekeza nguvu za kutwaa mgodi wa Kiwira ulianza kwenye nia ovu, yaani kujitwalia mali ya umma bila kufuata njia za wazi za zabuni zinazojulikana. Huu ni ovu.

Lakini uovu huu unakuwa mbaya zaidi kwa sababu, kiongozi mkuu wa nchi yeye binafsi, mkewe na watoto wake, bila kusahau waziri wake na mwanae walijiunga pamoja katika kutafakari nia ovu, na mwishowe ni kujichukulia Kiwira kwa hila. Ni hila kwa sababu walijua fika hawana uwezo wa kifedha, kitekinolojia waka utaalaam wa kuukwamua mgodi huo, mbali tu ya kujipanga kwa nia ya kuikamua Tanesco na taasisi nyingine za fedha nchini kama walivyochotewa mabilioni ya NSSF ili wawekeze Kiwira, lakini hadi leo hakuna ushahidi wa matumzi sahihi ya fedha hizo.

Ndiyo maana wale wote wanaojitokeza kumtetea Mkapa katika haya machafu yake, wanakosa ujasiri wa kizalendo kuona kwa macho maangavu kwamba katika matendo ya kiongozi huyo, aliongozwa na nia ovu kwenye suala zima la Kiwira.

Kwa hiyo utetezi wa eti hakulipia hisa zake hauwezi kumsafisha kwa sasa; lakini la muhimu zaidi ni tabia yake mwenyewe (Mkapa) kujikalia kimya kama kwamba yanayosemwa na kuandikwa dhidi yake ni ya kumdhalilisha na kumuonea kwa kuwa yu msafi!

Serikali nayo kwa kushindwa kusoma alama za nyakati imeingia kwenye jukumu la kumsafisha Mkapa, bila kujiuliza kama ilikuwa ni haki kwa kiongozi huyo kwanza kushiriki kisirisiri kuwania kununua mali ya umma ambayo amekabidhiwa kuilinda na kuitunza; kubwa zaidi kuwaalika hata wale wa nyumbani kwake kushiriki katika uovu huu.

Tunasikitika serikali inapoteza nguvu na rasilimali nyingine za maana kutafuta njia ya kumnusuru Mkapa wakati ikijua wazi kiongozi huyu alinuia kutenda uovu dhidi ya kiapo chake cha urais; alithubutu kutumia Ikulu kujitafutia kipato binafsi tena kwa uficho, lakini baya zaidi kiongozi huyu hajaonekana kujutia makosa yake ila anaendeleza malumbano kana kwamba anaonewa na baadhi ya vyombo vya habari. Rejea kauli yake kijijini kwake Lupaso kwamba magazeti yanasema uongo, uongo, uongo, uongo, uongo!

Ni kwa kutafakari hali hii nadiriki kuwauliza watetezi wa Mkapa kwamba watatumia sabuni gani ili atakasike kama mwenyewe amekataa kuoga?

spot_img

Latest articles

Balozi Nchimbi awafariji Mzee Makamba na Familia ya Mwambi

Na Mwandishi Wetu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amemtembelea...

Mtanzania achaguliwa Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Dunia

Na Mwandishi Maalum, Washington D.C Benki ya Dunia imemchagua Mtanzania, Dk. Zarau  Kibwe, kuwa Mkurugenzi...

Shamba darasa kutoka Kenya: Hata Rais anatokwa jasho

KUNA kitu kinaitwa ‘shamba darasa’. Hili ni shamba ambalo huandaliwa na kuendeshwa kwa nia...

Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi yaanza kazi, yakaribisha wananchi kutoa maoni

Na Winfrida Mtoi Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza...

More like this

Balozi Nchimbi awafariji Mzee Makamba na Familia ya Mwambi

Na Mwandishi Wetu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amemtembelea...

Mtanzania achaguliwa Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Dunia

Na Mwandishi Maalum, Washington D.C Benki ya Dunia imemchagua Mtanzania, Dk. Zarau  Kibwe, kuwa Mkurugenzi...

Shamba darasa kutoka Kenya: Hata Rais anatokwa jasho

KUNA kitu kinaitwa ‘shamba darasa’. Hili ni shamba ambalo huandaliwa na kuendeshwa kwa nia...