Na Jesse Kwayu
UKIFUATILIA vyombo vya habari vya Kenya unaweza kudhani kwamba mwaka huu watakuwa na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge, lakini ukweli ni kwamba uchaguzi wao wanautarajia mwaka 2022. Tanzania tutakuwa na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge Oktoba mwaka huu. Kwa bahati mbaya hakuna mwamko wowote wa maana kwamba mwaka huu ni wa uchaguzi.
Kenya ni nchi ya harakati za kisiasa, uchaguzi mkuu mmoja ukiisha harakati za uchaguzi mkuu mwingine huanza hata kabla walioshinda uchaguzi hawajaanza kutekeleza majukumu yao. Unaweza kuelezea siasa za Kenya kama taifa linalozungumza wakati wote. Hisia za wananchi zinajitokeza wakati wote juu ya waliochaguliwa na ambao wangependa wachaguliwe kipindi kingine. Ni nchi ambayo siasa ni haki halali ya kila raia.
Hapa kwetu Tanzania miaka ya nyuma hasa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 kidogo kidogo taifa lilianza kuchemka katika uwanda wa siasa. Watu wakaanza kuzungumza, hisia za wananchi zikawa zinaonekana dhahiri, vyama vingi vya siasa vikafumuka. Hata hivyo, baada ya chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015, kila kipindi taifa hili likashuhudia aina tofauti ya msisimko wa kisiasa ndani ya jamii.
Kwamba watu wako huru kujiunga na vyama vya siasa watakavyo hadi leo siyo tatizo; kwamba kila chama kina uhuru na haki ya kushiriki katika uchaguzi kuanzia wa serikali za mitaa hadi wa kitaifa nalo pia halijawahi kuwa shida, isipokuwa katika miaka ya hivi karibuni zimeanza kuibuka siasa za utengano. Kwamba kidogo kidogo siasa zetu zinaanza kuegemea upande mmoja. Kwamba mwenye dola ndiye anaamua nani afanye siasa wakati gani na kwa nini? Siyo sheria tena. Hali hii inaweza kuanza kujenga ufa katika taifa.
Ni kwa nini hali hii inaweza kujenga ufa? Siasa ni msingi mkuu wa maamuzi ya jinsi taifa husika linavyoamua mgawanyo wa keki ya taifa. Siasa ni juu ya maamuzi ya mgawanyo wa rasilimali za taifa, ni juu ya bajeti ya nchi, halmashauri na hata kijiji. Kwa maneno mengine siasa ni uamuzi wa pamoja kwa waliopewa madaraka kuamua mipango ipi ya maendeleo itekelezwe, itekelezwe wapi na kwa rasilimali zipi. Siasa ni mfumo wa maisha ya binadamu juu ya maamuzi ya hatma yao. Ni uamuzi wa nani apate nini na kwa wakati gani. Mgawanyo.
Hata hivyo, pamoja na haki ya walioshinda kuongoza, bado haki ya walioshindwa haipotee. Wana haki ya kuhoji maamuzi, kuibua changamoto, kukosoa na kutoa mawazo mbadala. Hayo huwapa naouhalali wa kushiriki siasa. Kwa kumombo tungesema wana haki ya critique. Na nayepigwa critique asifure na kutaka kuwafuga watu mdomo. Afanye kazi kwa sababu mwenye kutoa ridhaa ni mwananchi.
Ni kwa maana hiyo pia, unapokuwa na mfumo wa kisiasa wa anayeshinda kuchukua kila kitu (winner takes all) bila kuwa na utaratibu wa hata kutaka kusikia ni mbadala wa kinachotekelezwa, haishangazi kujengeka kwa mfumo wa siasa wa kusigana wakati wote.
Kuna watu wangetamani sana kuona kwamba taifa hili linarejea kwenye mfumo wa chama kimoja. Wanaamini kwamba vyama vingi ni uasi, usaliti na pengine ni vurugu kwa wananchi. Mawazo haya yamejengwa kwenye msingi mbaya wa kulelea na kuendesha siasa zetu. Kwamba dhana ya winner takes all imekuwa tamu mno kwa wanaoshinda hata pale ushindi wenyewe ni mdogo sana.
Kwa mfano, ukitafakati kila uchaguzi mkuu unaofanyika Zanzibar, siyo wakai huu wa kujitawalawenyewe tu, bali hata tangu zama za ukoloni, jamii ile ni kama imejigawa kati kwa kati. Je, siasa za kufaa pale ni za winner takes all tu? Je, mgawanyo wa rasilimali za umma unaweza kufanywa na nusu moja tu ya jamii na nchi ikatulia.
Ukijiuliza kwa mfano, ni kwa nini miaka ya hivi karibuni watu wazito wenye taaluma zao kama maprofesa au madaktari au wahandisi au walimu au wahasibu yaani mwenye kazi katika taaluma yoyote wanakimbilia kwenye siasa? Jibu ni jepesi sana, siasa inalipa kuliko huko waliko.
Upo uthibitisho kwamba watu wanauza hata mali zao zenye thamani kubwa kama nyumba, magari, mashamba na viwanja ili wapate fedha za kuwekeza kwenye siasa. Ili wafanikiwe kuchagulia ama kuwa mbunge au diwani na hata mwenyekiti wa serikali za mitaa. Jambo la kujiuliza ni hili, je, kuna faida ya kiasi gani katika siasa kiasi cha kushawishi mtu kuuza mali zake? Je, vitu hivyo alivyoamua kuuza atavirejesha vipi? Au siasa ni huduma tu kwa jamii kwa maana hiyo wauza mali zao wameamua kujitosa kwenye utumishi wa kutumikia umma bila faida binafsi yoyote?
Utayari wa watu kutumia rasilimali zao kiasi hicho ndio unathibitisha kuwa siasa ni mchezo ambazo unahitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Umakini wa kuhakikisha kwamba jamii kwa ujumla wake haiathiriwi na maamuzi ya wachache au wengi waliopata fursa ya kukalia ofisi za umma za kuchaguliwa.
Mizozo mingi ambayo imeshuhudiwa katika nchi nyingi, hasa za Afrika, Asia na Amerika ya Kusini chimbuko lake ni kuruhusu kuchezwa kwa mchezo wa siasa katika mfumo ambao umma unatengwa na unufaikaji wa keki ya taifa. Kwa maana hiyo, tunapoona majirani zetu wakiendesha harakati za siasa wakati wote, ni kielelezo cha kutambua kuwa mapambano ya mgawanyo wa keki ni makubwa sana katika mfumo wa kisiasa wa mshindi kubeba kila kitu (winner takes all).
Katika muktadha kama huu, tunapoitazama Tanzania na mfumo wetu wa kisiasa wa winner takes all yatupasa kuutafakari ili kujenga wigo mpana wa jinsi ya umma utanufaika na mgawanyo wa keki ya taifa. Tutafute siasa za ushirikishwaji wote (inclusiveness).