MSIGWA ATAKA HABARI ZA VIJIJINI KUPEWA KIPAUMBELE

Na Tatu Mohamed

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewataka waandishi wa habari nchini kuimarisha uandishi wa habari za vijijini kwa kufanya tafiti na kuibua changamoto pamoja na fursa zinazowakabili wananchi ili kuhakikisha sauti zao zinasikika.

Amesema licha ya takribani asilimia 65 ya Watanzania kuishi vijijini, zaidi ya asilimia 80 ya vyombo vya habari viko mijini, hali inayochangia habari nyingi kuelekezwa kwenye matukio ya mijini na kuacha changamoto na maendeleo ya wananchi wa vijijini bila kupewa nafasi inayostahili.

Msigwa ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano vijijini nchini Tanzania na Mkutano Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Vijijini Tanzania (RUJAT)Msigwa amesema ni muhimu vyombo vya habari kubadilisha mtazamo na kuelekeza nguvu katika habari zinazogusa maisha ya wananchi.

“Uandishi wa habari za vijijini haupaswi kujikita katika kuripoti taarifa za viongozi pekee, bali kuangazia maisha ya wananchi, shughuli zao za kiuchumi, changamoto na fursa zinazoweza kuboresha ustawi wao,” amesema.

Ametoa mfano wa fursa za kilimo, akieleza kuwa taarifa kuhusu uwezekano wa kulima zao la tufaha (apple) mkoani Dodoma ni miongoni mwa habari zinazoweza kuwasaidia wakulima kutambua fursa mpya za kuongeza kipato na uzalishaji.

Aidha, amewataka waandishi wa habari kurejesha misingi ya taaluma hiyo kwa kufanya utafiti, kujenga ushindani wa kihabari na kuhakikisha wanakusanya taarifa za kutosha kabla ya kuandika habari, akisema ubora wa habari unategemea juhudi na weledi wa mwandishi.

Amesema kupungua kwa imani ya wananchi kwa vyombo vya habari ni jambo linalopaswa kufanyiwa utafiti ili kubaini sababu zake, akisisitiza kuwa jukumu la kuwahabarisha wananchi linapaswa kubaki mikononi mwa waandishi wa habari wenye weledi na wanaozingatia misingi ya taaluma.

Msigwa pia ameonya kuhusu waandishi wa habari kuwekwa kwenye makundi yenye maslahi maalumu, akisema hali hiyo inaweza kuathiri uhuru, uhuru wa maamuzi na uwezo wa mwandishi kusimamia maslahi ya umma bila upendeleo.

Kuhusu mazingira ya kazi, amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za kiuchumi zinazovikabili vyombo vya habari, ikiwemo madeni yanayotokana na huduma zilizotolewa kwa taasisi za Serikali, huku akieleza kuwa baadhi ya malipo yanaendelea baada ya kukamilishwa kwa nyaraka zinazohitajika.

“Serikali pia inaandaa maboresho ya kanuni za Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, ikiwemo mapendekezo ya kuweka utaratibu wa mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi wa habari ili kuwawezesha kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la habari,” amesema.

Katika hatua nyingine, Msigwa amewataka waandishi wa habari kuzingatia masuala ya usalama wa taifa katika kazi zao, akisema taarifa zina nguvu kubwa katika kujenga au kuathiri jamii, hivyo ni muhimu kuzingatia athari za habari kabla ya kuzichapisha.

Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wanahabari katika kutatua changamoto zao na kueleza kuwa imepanga kujenga Kituo cha Habari Tanzania jijini Dodoma kitakachokuwa na maeneo maalumu ya kufanyia kazi kwa waandishi wa habari watakaokuwa katika shughuli za kikazi mjini humo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema ushirikiano unaooneshwa na viongozi wa Serikali, hususan Msigwa, unatoa fursa ya kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na waandishi wa habari katika kutatua changamoto zinazowakabili wanahabari.

Amesema ni muhimu waandishi wa habari za vijijini kujengewa uwezo katika kuandaa na kuwasilisha habari zenye ubora, akibainisha kuwa zipo habari zenye hoja na taarifa muhimu lakini zinakosa nguvu kutokana na namna zinavyoandaliwa na kuwasilishwa kwa wasomaji au wasikilizaji.

Meena amewataka viongozi wa taasisi za Serikali na maofisa habari kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari wanapohitaji taarifa, akisisitiza kuwa wanahabari si maadui wa Serikali bali ni wadau muhimu katika kuhabarisha jamii na kuibua masuala yanayohitaji ufumbuzi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Bunda, Esther Bulaya, aliwataka waandishi wa habari kurejesha ushindani wa kitaaluma kwa kufanya kazi kwa bidii, kuimarisha uandishi wa habari za uchunguzi na kujenga uwezo wa kuibua habari zenye manufaa kwa jamii.

Bulaya, ambaye pia ni mwandishi wa habari kitaaluma, amesema mafanikio yake katika safari ya uongozi yametokana kwa sehemu kubwa na misingi ya taaluma aliyojifunza kwa waandishi waliomtangulia, akisisitiza umuhimu wa waandishi wenye uzoefu kuwajenga na kuwaongoza vijana wanaoingia katika tasnia hiyo.

“Waandishi wanapaswa kujifunza zaidi ya kuripoti matukio ya kawaida kwa kuibua masuala yanayohitaji uchunguzi na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi yanayogusa maisha ya wananchi,” amesema.

Awali, Katibu Mkuu wa RUJAT, Prosper Kwigize, amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 2020 baada ya waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali kukutana na kuona umuhimu wa kuwa na jukwaa maalumu la kuimarisha uandishi wa habari za vijijini.

Amesema RUJAT ilianza na wanachama 20 na kwa sasa ina wanachama 120, huku ikiwa na maombi mengine zaidi ya 60 kutoka kwa waandishi wanaotaka kujiunga na chama hicho.Kwigize amesema RUJAT inalenga kujenga uwezo wa wanachama, kutetea uhuru wa vyombo vya habari, kuimarisha upatikanaji wa taarifa na kuhakikisha habari za vijijini zinapata nafasi katika vyombo vya habari nchini.

Ameongeza kuwa chama hicho kinahamasisha uandishi unaozingatia maadili, ushirikishwaji wa jamii na ubunifu katika kutafuta habari, huku kikilenga kuhakikisha taarifa zinazotolewa zinakuwa na matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

spot_img

Latest articles

MKUU WA WILAYA YA LUDEWA AWATAKA VIONGOZI KUWA MABALOZI WA ELIMU YA FEDHA NCHINI

Na Mwandishi wetu, Njombe MKUU wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, 8amewahimiza viongozi wa wilaya...

NeST yawezesha Zabuni za Sh Trilioni 42.6, serikali yaokoa Sh. Bilioni 28

Na Tatu Mohamed MFUMO wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni...

TANZANIA, ANGOLA KUFUNGUA NJIA MPYA ZA BIASHARA

Na Tatu Mohamed RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano...

WANANCHI TABORA NA KATAVI KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA, TANESCO YAANZA UFUNGAJI WA TRANSFOMA YA MVA 150

📌 Ni sehemu ya Utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi,...

More like this

MKUU WA WILAYA YA LUDEWA AWATAKA VIONGOZI KUWA MABALOZI WA ELIMU YA FEDHA NCHINI

Na Mwandishi wetu, Njombe MKUU wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, 8amewahimiza viongozi wa wilaya...

NeST yawezesha Zabuni za Sh Trilioni 42.6, serikali yaokoa Sh. Bilioni 28

Na Tatu Mohamed MFUMO wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni...

TANZANIA, ANGOLA KUFUNGUA NJIA MPYA ZA BIASHARA

Na Tatu Mohamed RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano...