Na Tatu Mohamed
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kwa kuunganisha miundombinu ya usafiri, kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege na kuongeza fursa za uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema licha ya Tanzania na Angola kuwa na uhusiano wa kihistoria uliojengwa wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara bado ni mdogo, hivyo nchi hizo zimekubaliana kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na sekta binafsi kutafuta fursa za ushirikiano.

Rais Samia ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2026 jijini Dar es Salaam, baada ya mazungumzo ya nchi mbili na Rais wa Angola, João Lourenço, aliyeko nchini kwa ziara ya kitaifa.
Amesema hatua nyingine ni kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa kuunganisha Korido ya Lobito ya Angola na Korido ya Dar es Salaam pamoja na reli ya kati, sambamba na ukarabati wa reli ya TAZARA na Reli ya Benguela ya Angola.
Amesema kukamilika kwa mipango hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, kuongeza biashara na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika.
Aidha, nchi hizo zimesaini makubaliano ya huduma za usafiri wa anga yatakayowezesha kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kati ya nchi hizo, hatua inayotarajiwa kuchochea biashara, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika sekta ya nishati, Rais Samia amesema Tanzania imeanza mchakato wa kutathmini uwezekano wa kushiriki katika uwekezaji wa mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Angola kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Pia, Nchi hizo zimekubaliana kubadilishana uzoefu katika sekta ya madini, kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na wataalamu pamoja na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa.
Amesema Tanzania pia imeamua kufungua tena ubalozi wake nchini Angola ili kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za ushirikiano kati ya nchi hizo.

Ameeleza kuwa mataifa hayo yamejadili pia ushirikiano katika afya, hususan afya ya mama na mtoto, elimu na masuala ya amani na usalama wa kikanda.
Kwa upande wake, Rais Lourenço amesema Tanzania na Angola zina historia ya urafiki na mshikamano iliyojengwa wakati wa mapambano ya ukombozi wa Afrika, hivyo ni wakati wa kuimarisha uhusiano huo kwa kuupanua katika biashara, uwekezaji, usafiri na sekta nyingine za maendeleo.
Amesema kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kutaziwezesha nchi hizo kunufaika kwa pamoja na fursa zilizopo katika mataifa yao.Katika ziara hiyo, nchi hizo pia zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali, yakiwamo huduma za usafiri wa anga, mawasiliano na hali ya hewa, pamoja na makubaliano mengine yaliyotangazwa na pande hizo.



