NeST yawezesha Zabuni za Sh Trilioni 42.6, serikali yaokoa Sh. Bilioni 28

Na Tatu Mohamed

MFUMO wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni 403,643 zenye thamani ya Sh trilioni 42.6 na kuiwezesha Serikali kuokoa takribani Sh bilioni 28 kupitia kupunguza matumizi ya karatasi na nyaraka za ununuzi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dennis Simba, amesema hayo Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OR-Treasury).

Amesema mafanikio mengine ya mfumo huo ni kuongezeka kwa kiwango cha uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa umma kutoka asilimia 65 katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi asilimia 79 mwaka 2025/26, kutokana na hatua mbalimbali za udhibiti, ikiwemo kuwafungia baadhi ya kampuni zilizokiuka sheria.

Simba amesema mfumo huo pia umepunguza muda na gharama za usafiri kwa wazabuni, kwa kuwa sasa wanaweza kupata taarifa za zabuni na kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi za taasisi husika.

Ameongeza kuwa zaidi ya benki 36 zimeunganishwa na Mfumo wa Bank Security Portal ili kurahisisha utoaji na uhakiki wa dhamana za zabuni, huku watumiaji wakihimizwa kutumia programu ya NeST Tender inayopatikana Play Store na App Store kufuatilia taarifa za zabuni na hali ya malipo.

Akizungumzia fursa zinazotokana na mfumo huo, Simba amesema makundi maalum yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu yamepata zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 82.34, hatua inayowawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi kupitia ununuzi wa umma.

Amesema vijana wamepata zabuni zenye thamani ya Sh bilioni 44.74, wanawake Sh bilioni 33.51, wazee Sh bilioni 3.78, huku watu wenye ulemavu wakipata zabuni zenye thamani ya Sh milioni 680.

Amesema hadi sasa makundi maalum 33,659 yamesajiliwa katika mfumo huo na kupata fursa za kufanya kazi mbalimbali za Serikali, zikiwemo ujenzi, usafi na utengenezaji wa madawati ya shule.

Simba amesema PPRA inaendelea kutoa elimu kwa makundi hayo ili kuyawezesha kuelewa taratibu za ununuzi wa umma na namna ya kutumia mfumo wa NeST kupata zabuni zinazotangazwa na taasisi za Serikali.

Amesema mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa umma kwa lengo la kuimarisha uwazi, ushindani wa haki na kuongeza ushiriki wa wazawa katika zabuni za Serikali ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kukuza uchumi wa taifa.

Akizungumzia manufaa ya mfumo huo kwa makundi maalum, Mwenyekiti wa Kikundi cha Nyota Bora, Godwin Mmisi, amesema elimu inayotolewa na PPRA imeongeza uelewa wao kuhusu fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.

Mmisi, ambaye pia anaongoza vikundi vinavyojihusisha na shughuli za ubebaji mizigo katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Ubungo, amesema awali makundi hayo yalikuwa yakikabiliwa na changamoto ya kutambua namna ya kupata fursa zilizotengwa kwa ajili yao.

Amesema elimu na ufafanuzi wanaopata kutoka PPRA umewasaidia kuelewa taratibu za kuingia katika mifumo ya ununuzi wa umma na namna ya kushiriki katika zabuni mbalimbali.

“Tunashukuru Serikali kwa kutupatia fursa hizi. PPRA imekuwa ikitusaidia kwa kutupatia elimu na ufafanuzi kuhusu namna ya kutumia mifumo hiyo ili nasi tuweze kunufaika na fursa za kiuchumi,” amesema Mmisi.

Ameongeza kuwa wanachama wa vikundi hivyo wanaendelea na shughuli za kubeba mizigo katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli, Ubungo, na kupata kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.

spot_img

Latest articles

TANZANIA, ANGOLA KUFUNGUA NJIA MPYA ZA BIASHARA

Na Tatu Mohamed RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano...

WANANCHI TABORA NA KATAVI KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA, TANESCO YAANZA UFUNGAJI WA TRANSFOMA YA MVA 150

📌 Ni sehemu ya Utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi,...

SELF MF YATOA MIKOPO YA SH BILIONI 138

Na Tatu Mohamed MFUKO wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umetoa...

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA BANDA LA TANESCO KATIKA HAFLA YA UTIAJI SAINI LESENI ZA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI

📌Aelezwa jinsi TANESCO inavyozalisha Umeme kupitia Vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo gesi asilia Na Mwandishi...

More like this

TANZANIA, ANGOLA KUFUNGUA NJIA MPYA ZA BIASHARA

Na Tatu Mohamed RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano...

WANANCHI TABORA NA KATAVI KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA, TANESCO YAANZA UFUNGAJI WA TRANSFOMA YA MVA 150

📌 Ni sehemu ya Utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi,...

SELF MF YATOA MIKOPO YA SH BILIONI 138

Na Tatu Mohamed MFUKO wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umetoa...