Na Tatu Mohamed
MFUKO wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umetoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 138 kwa wanufaika 131,312 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023 hadi 2026, huku mikopo hiyo ikitajwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kuzalisha ajira 262,624 nchini.
Hayo yameelezwa na leo Oktoba 28, 2026 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Santieli Yona, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mfuko katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha mchango wa taasisi hiyo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapatia mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara.
Amefafanua kuwa, katika kipindi hicho, mfuko umepata faida ya Sh bilioni 3.19 na kutoa gawio la Sh milioni 490 kwa Serikali, hatua inayoonesha uwezo wake wa kujiendesha kibiashara huku ukiendelea kutekeleza jukumu la kijamii la kuwezesha wananchi kupata huduma za kifedha.
“Mfuko unaendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi mengine ya wananchi, pamoja na taasisi za kifedha zikiwemo Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na Vyama vya Ushirika vya Mazao (AMCOS), ili kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wanachama wake,” amesema.
Amesema baadhi ya wanufaika wameweza kupanua biashara zao na kuongeza uwezo wa kukopa baada ya kuanza na mikopo midogo, huku mfuko ukitoa pia mikopo ya maendeleo ya makazi kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba na mikopo kwa watumishi wa umma.
Aidha, amesema SELF imeweka bidhaa maalumu za mikopo zinazowawezesha vijana kumiliki vyombo vya usafiri, ikiwemo bajaji, kwa ajili ya kujiajiri na kuongeza kipato. Hatua hiyo inalenga kupanua fursa za ajira na kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
Katika kuongeza upatikanaji wa huduma, amesema mfuko una mtandao wa matawi 12 na vituo viwili vya huduma vilivyofunguliwa mikoa ya Kigoma na Katavi, huku ukiendelea kuhudumia wananchi katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema katika mpango wa miaka mitano ijayo, mfuko unalenga kuimarisha huduma za kidijitali ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa na huduma za mikopo kwa urahisi bila kulazimika kufika katika matawi yake, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto za umbali na kuongeza ufanisi wa huduma.
Kuhusu uhifadhi wa mazingira, amesema mfuko unatoa mikopo inayowawezesha wananchi kupata majiko yanayotumia umeme kwa kiwango kidogo, pamoja na bidhaa nyingine zinazohamasisha matumizi ya nishati safi na kulinda mazingira.
Ameongeza kuwa mfuko unaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wanufaika kabla na baada ya kupatiwa mikopo ili kuwasaidia kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, kupanga marejesho na kuendesha biashara zao kwa ufanisi.
Hata hivyo, amesema changamoto zinazoukabili mfuko ni pamoja na uelewa mdogo wa elimu ya fedha kwa baadhi ya wananchi, kutorejeshwa kwa mikopo kwa wakati na biashara nyingi za wajasiriamali wadogo kutokuwa rasmi.
Amesema mfuko unaendelea kutoa elimu, kuhamasisha urasimishaji wa biashara na kuwashauri wateja kuzingatia taratibu zinazohitajika ili kuongeza fursa za kupata huduma za kifedha na kuhakikisha mikopo inatumika kukuza biashara, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.


