TANZANIA, ANGOLA KUFUNGUA NJIA MPYA ZA BIASHARA

Na Tatu Mohamed

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Angola zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kwa kuunganisha miundombinu ya usafiri, kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege na kuongeza fursa za uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.

Amesema licha ya Tanzania na Angola kuwa na uhusiano wa kihistoria uliojengwa wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara bado ni mdogo, hivyo nchi hizo zimekubaliana kuandaa kongamano la biashara na uwekezaji litakalowakutanisha wafanyabiashara na sekta binafsi kutafuta fursa za ushirikiano.

Rais Samia ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2026 jijini Dar es Salaam, baada ya mazungumzo ya nchi mbili na Rais wa Angola, João Lourenço, aliyeko nchini kwa ziara ya kitaifa.

Amesema hatua nyingine ni kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji kwa kuunganisha Korido ya Lobito ya Angola na Korido ya Dar es Salaam pamoja na reli ya kati, sambamba na ukarabati wa reli ya TAZARA na Reli ya Benguela ya Angola.

Amesema kukamilika kwa mipango hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu, kuongeza biashara na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika ukanda wa Afrika.

Aidha, nchi hizo zimesaini makubaliano ya huduma za usafiri wa anga yatakayowezesha kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kati ya nchi hizo, hatua inayotarajiwa kuchochea biashara, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi.

Katika sekta ya nishati, Rais Samia amesema Tanzania imeanza mchakato wa kutathmini uwezekano wa kushiriki katika uwekezaji wa mradi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Angola kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Pia, Nchi hizo zimekubaliana kubadilishana uzoefu katika sekta ya madini, kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na wataalamu pamoja na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa.

Amesema Tanzania pia imeamua kufungua tena ubalozi wake nchini Angola ili kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za ushirikiano kati ya nchi hizo.

Ameeleza kuwa mataifa hayo yamejadili pia ushirikiano katika afya, hususan afya ya mama na mtoto, elimu na masuala ya amani na usalama wa kikanda.

Kwa upande wake, Rais Lourenço amesema Tanzania na Angola zina historia ya urafiki na mshikamano iliyojengwa wakati wa mapambano ya ukombozi wa Afrika, hivyo ni wakati wa kuimarisha uhusiano huo kwa kuupanua katika biashara, uwekezaji, usafiri na sekta nyingine za maendeleo.

Amesema kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kutaziwezesha nchi hizo kunufaika kwa pamoja na fursa zilizopo katika mataifa yao.Katika ziara hiyo, nchi hizo pia zimesaini makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali, yakiwamo huduma za usafiri wa anga, mawasiliano na hali ya hewa, pamoja na makubaliano mengine yaliyotangazwa na pande hizo.

spot_img

Latest articles

NeST yawezesha Zabuni za Sh Trilioni 42.6, serikali yaokoa Sh. Bilioni 28

Na Tatu Mohamed MFUMO wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni...

WANANCHI TABORA NA KATAVI KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA, TANESCO YAANZA UFUNGAJI WA TRANSFOMA YA MVA 150

📌 Ni sehemu ya Utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi,...

SELF MF YATOA MIKOPO YA SH BILIONI 138

Na Tatu Mohamed MFUKO wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umetoa...

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA BANDA LA TANESCO KATIKA HAFLA YA UTIAJI SAINI LESENI ZA UTAFUTAJI WA MAFUTA NA GESI

📌Aelezwa jinsi TANESCO inavyozalisha Umeme kupitia Vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo gesi asilia Na Mwandishi...

More like this

NeST yawezesha Zabuni za Sh Trilioni 42.6, serikali yaokoa Sh. Bilioni 28

Na Tatu Mohamed MFUMO wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umewezesha kutolewa kwa zabuni...

WANANCHI TABORA NA KATAVI KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA, TANESCO YAANZA UFUNGAJI WA TRANSFOMA YA MVA 150

📌 Ni sehemu ya Utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi,...

SELF MF YATOA MIKOPO YA SH BILIONI 138

Na Tatu Mohamed MFUKO wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha (SELF Microfinance Fund) umetoa...