KAMPUNI ya Zara Tanzania Adventures imezindua rasmi kampeni ya Twenzetu Kileleni – Msimu wa Tano, inayolenga kuhamasisha Watanzania kushiriki utalii wa ndani kwa kupanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo, Septemba 10, 2026, katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika.
Kupitia kampeni hiyo, Watanzania wanahamasishwa kutembelea Mlima Kilimanjaro kupitia njia ya Marangu na kufurahia mojawapo ya hazina kubwa za Tanzania na Afrika, Kilele cha Uhuru kinachotajwa kuwa Paa la Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Zara Tanzania Adventures, Zainab Ansell, amesema msimu wa tano unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya watu 200 watakaopanda Mlima Kilimanjaro, huku vijana watakaowaunga mkono wakifanya idadi ya washiriki kufikia zaidi ya 400.
Ansell amesema kampeni hiyo inalenga kuwafanya Watanzania kutambua na kuthamini vivutio vya utalii vilivyopo nchini, akibainisha kuwa wageni kutoka nje ya nchi wamekuwa wakifika kwa wingi kupanda Mlima Kilimanjaro.
“Wageni kutoka nje ya nchi wamekuwa wakifika kwa wingi kupanda Kilimanjaro, hivyo ni wakati kwa Watanzania wenyewe kutumia fursa hiyo kujivunia rasilimali zao,” amesema Ansell.

Amesema kabla ya kuanza safari ya kupanda mlima, washiriki watashirikishwa katika shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo upandaji miti, kwa lengo la kuhakikisha Mlima Kilimanjaro unaendelea kuwa rasilimali salama kwa vizazi vijavyo.
Kwa Watanzania ambao hawataweza kupanda mlima, Ansell amesema watapata fursa ya kuungana na wenzao katika safari za kutembelea maeneo mengine ya utalii, yakiwemo Hifadhi za Taifa za Serengeti, Lake Manyara na Ngorongoro.
Amesema hatua hiyo itawapa wananchi fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa gharama nafuu, huku Zara Tanzania Adventures ikiendelea kushirikiana na jamii kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo kusaidia elimu na upandaji miti.
Ansell amewataka Watanzania kutumia mwezi Desemba kutembelea Mlima Kilimanjaro na Serengeti ili kujionea utajiri wa utalii uliopo nchini.

Kwa upande wake, Faustine John kutoka Zara Tanzania Adventures amesema kampuni hiyo imejiandaa kuhakikisha washiriki wanapata huduma bora wakati wa safari, zikiwemo mavazi, malazi, chakula, waongozaji wenye ujuzi pamoja na elimu kuhusu mazingira na rasilimali zinazopatikana katika eneo la Kilimanjaro.
Amesema njia ya Marangu imechaguliwa kwa kuwa ina miundombinu ya malazi na inafaa kwa kipindi cha mvua kinachotarajiwa, huku washiriki wakipanga kutumia siku sita katika safari hiyo ili kupata nafasi ya kufurahia mazingira na kufikia kilele.
Ametoa wito kwa viongozi wa Serikali, wabunge, mawaziri, taasisi binafsi, taasisi za dini, mabalozi na Watanzania kwa ujumla kujitokeza na kushiriki programu hiyo ili kuonyesha mfano katika matumizi ya vivutio vya utalii vya ndani.
“Tunawahamasisha viongozi wa Serikali, wabunge, mawaziri, taasisi binafsi, taasisi za dini, mabalozi na Watanzania kwa ujumla kujitokeza na kushiriki programu hii,” amesema.
Ameongeza kuwa Zara Tanzania Adventures ina uzoefu wa miaka 40 katika kuendesha shughuli za utalii na imejiandaa pia kutoa huduma kwa watu wenye mahitaji maalumu wanaotaka kushiriki safari za utalii.
Naye Afisa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Albert Mboto, amesema juhudi zinazofanywa na Zara Tanzania Adventures zina mchango katika kuendeleza utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza sekta hiyo.

Mboto amesema wadau mbalimbali wanapaswa kutumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii na kuunga mkono juhudi zinazolenga kukuza sekta hiyo.“Hii ni fursa ya kuhamasisha kampuni na wananchi mbalimbali kuunga mkono juhudi zinazolenga kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kuinuka,” amesema Mboto.
Naye Peter Mwambuga kutoka TTCL amesema huduma za mawasiliano zimeboreshwa katika eneo la Mlima Kilimanjaro, ikiwemo uwezo wa mawasiliano kuanzia lango la Marangu hadi kileleni.
Amesema maboresho hayo yatasaidia washiriki kupata huduma za mawasiliano wakati wa safari na kurahisisha mawasiliano wanapokuwa mlimani.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Mary Maduhu, amesema kampeni hiyo ni fursa muhimu kwa wanafunzi na wafanyakazi kupata uzoefu wa moja kwa moja katika utalii wa milimani, uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa urithi wa Taifa.
Kampeni ya Twenzetu Kileleni – Msimu wa Tano imezinduliwa wakati Tanzania ikielekea kusherehekea miaka 65 ya Uhuru wa Tanganyika, huku waandaaji wakihamasisha Watanzania kutumia maadhimisho hayo kuitembelea Tanzania, kuifahamu na kuthamini urithi wake.
Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni “Twenzetu Kileleni Msimu wa Tano – Miaka 65 ya Uhuru. Taifa Moja. Kilele Kimoja. Paa la Afrika.”


