Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetangaza kusitishwa kwa huduma ya maji kwa takribani saa 12 katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani, kesho Alhamisi, Septemba 10, 2026.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi Everlasting Lyaro amesema huduma itakatika kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, kutokana na matengenezo kinga ya miundombinu ya maji katika Mtambo wa Ruvu Juu uliopo Kibaha, yanayolenga kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa.

Amesema maeneo yatakayoathirika kutokana na matengenezo haya ni pamoja na Ruvu Darajani, Ruvu JKT, Vigwaza, Mlandizi, Mbwawa, Soga, Mwendapole, Tanita, Kwa Mathias, Picha ya Ndege, Kibaha, Kiluvya, Kibamba, Malamba Mawili, Saranga, Mbezi, Ubungo, Kimara, Tabata, Segerea, Kinyerezi, Kisukuru, Bonyokwa, Ukonga, Uwanja wa Ndege, Kiwalani, Vingunguti, Gongo la Mboto, Pugu na Kisarawe.

Mamlaka imewataka Wananchi wa maeneo hayo kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi muhimu wakati wa matengenezo, huku ikiomba ushirikiano wao ili kazi hiyo ikamilike kwa ufanisi.


