Kampuni ya Rashal Energies Limited, chini ya Afisa Mtendaji Mkuu Farhiya Warsame, yajenga bomba la kilomita 22 kwa fedha, wahandisi na wafanyakazi wa Kitanzania, likilenga viwanda zaidi ya kumi, kituo cha DART Mbagala, na mtandao wa vituo vya gesi ya CNG utakaobadilisha usafiri na nishati safi ya kupikia jijini Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu, Mbagala, DSM
TANZANIA imefikia hatua ya kihistoria katika mageuzi yake ya nishati. Kwa miaka mingi, mazungumzo kuhusu hazina kubwa ya gesi asilia nchini yalijikita zaidi kwenye uwezekano wa baadaye.
Leo, uwezekano huo unabadilika kuwa nishati halisi, safi na ya bei nafuu inayotumika barabarani, viwandani na majumbani.

Wakati Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likistahili sifa kubwa kwa kuweka dira ya kimkakati na msingi wa kisera, sifa za utekelezaji zinaelekea kwa kampuni za ndani zinazobadilisha dira hiyo kuwa miundombinu halisi ardhini, ikiongozwa na Rashal Energies Limited.
Ujenzi wa bomba la kilomita 22 kutoka Kisemvule hadi Mbagala ulianza rasmi Julai 28, 2026, baada ya vibali na idhini zote za kisheria kukamilika Mei 2026 na maandalizi ya awali kukamilika mwezi Juni mwaka huu.

Hadi sasa, kilomita mbili za bomba zimeshaunganishwa, kilomita moja na nusu zimechimbwa mfereji, na sehemu za kwanza tayari zimewekwa ardhini, kufunikwa na kufanyiwa majaribio kwa mafanikio. Kampuni inalenga kukamilisha ujenzi wa bomba zima ifikapo Januari 2027.
Kazi zinazofanyika ni pamoja na kuunganisha mabomba kwa mfumo wa butt-fusion, uchimbaji sahihi wa mifereji, uwekaji wa tepu za tahadhari, na majaribio ya shinikizo la maji hatua zote za kiufundi zikitekelezwa vizuri licha ya mazingira magumu ya mjini yenye shughuli nyingi.
Aidha kinachoutofautisha mradi huu si tu kile utakachosafirisha, bali ni nani anayeujenga. Bomba hili linatekelezwa kwa mtaji binafsi wa Kitanzania kikamilifu, na kila mkataba wa ujenzi kwenye njia hii umepewa makandarasi wa ndani.

Timu zinazofanya kazi za uunganishaji wa mabomba, uchimbaji wa mifereji, ufunikaji na majaribio ya shinikizo ni Watanzania, na usimamizi wa kihandisi eneo la mradi pia ni wa Kitanzania.
Hili ni jambo la maana kwa sekta ambayo, kihistoria, imekuwa ikitegemea zaidi utaalamu wa kigeni.
Ujenzi wa mabomba katika eneo la mjini lenye watu na miundombinu mingine ni kazi isiyovumilia makosa, inahitaji umakini, usimamizi madhubuti wa mifereji karibu na miundombinu hai ya maji, umeme na mawasiliano, pamoja na utaratibu wa majaribio usio na nafasi ya makosa.

Hadi sasa, mradi haujarekodi uharibifu wowote kwa miundombinu ya wahusika wengine, wala kiungo chochote kilichokamilika hakijahitaji kufanywa upya, rekodi iliyofikiwa na timu za ndani zikifuata taratibu za kimataifa.
Chini ya uongozi mahiri wa Farhiya Warsame, Afisa Mtendaji Mkuu wa Rashal Energies inathibitisha kuwa makampuni ya Kitanzania yana uwezo wa kiufundi, dira na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa na migumu ya miundombinu ya gesi.
Timu za mradi zimefanikiwa kuratibu kazi kwa ushirikiano na TANROADS (mmiliki mkuu wa njia), TANESCO, DAWASA na TTCL zikifikia rekodi safi na hakuna usumbufu wowote kwa miundombinu ya wahusika wengine, na hakuna ajali yoyote iliyosababisha upotevu wa muda wa kazi.
Kiwango hiki cha nidhamu ya kiutendaji kinaweka kiwango kipya kwa makampuni ya kihandisi ya ndani katika Afrika Mashariki.

Ujuzi unaojengwa kwenye mradi huu hauishii hapo. Uunganishaji wa mabomba kwa kuchomelea(welding), upimaji wa njia, majaribio ya uimara wa bomba na usimamizi wa miradi ya mjini ni ujuzi unaoweza kutumika katika kila mradi wa usambazaji gesi utakaohitajika nchini kwa miongo ijayo, huku wafanyakazi wanaofunzwa kwenye bomba la Kisemvule Mbagala wanawakilisha uwezo utakaobaki Tanzania.
Bomba hili litahudumia zaidi ya viwanda kumi kwenye ukanda wa Kisemvule Mbagala, likiwaunganisha kila mmoja kwenye gesi asilia badala ya dizeli na mafuta mazito kwa ajili kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura.
Kwa miaka mingi, viwanda vilivyopo Mbagala na maeneo jirani vimekuwa vikibeba gharama na usumbufu wa kusafirisha mafuta kwa malori, ujio wa bomba hili utabadilisha hilo na kuleta usambazaji endelevu wenye mita, kwa gharama ya chini kwa kila kipimo cha nishati na uzalishaji mdogo zaidi wa hewa chafu.
Ujenzi wa Kituo Kikuu (Mother Station) Mbagala:
Awamu ya Kwanza ya mkakati wa Rashal inajikita kwenye kituo kikuu cha Mbagala, kitakacho shindilia gesi moja kwa moja kutoka kwenye bomba kwa ajili ya kujaza magari na kupakia mzigo wa kusafirisha kwenda vituo vidogo.
Kituo Kidogo (Daughter Station) Vijibweni:
Ili kupambana na changamoto za kijiografia na kuhudumia viwanda katika maeneo ya Kigamboni, kituo maalum kinaanzishwa Vijibweni, kikihudumiwa na magari maalumu yenye gesi iliyoshindiliwa.
Awamu ya Pili:
Katika awamu itakayofuata, vituo vitano vya gesi asili(CNG) vitajengwa, ili kuwa na mtandao imara utakaopunguza gharama za mafuta kwa waendeshaji wa usafiri na kupunguza uchafuzi wa hewa jijini Dar es Salaam.
Kituo cha DART Mbagala:
Bomba hili pia litasambaza gesi asilia kwenye kituo cha mfumo wa mabasi ya mwendokasi (DART) kilichopo Mbagala. Mfumo wa DART husafirisha mamia kwa maelfu ya abiria kila siku, hivyo upatikanaji wa gesi kituoni hapo unafungua njia kwa mabasi kutumia CNG badala ya dizeli kupunguza gharama za uendeshaji na uchafuzi wa mazingira katika njia zenye shughuli nyingi zaidi jijini.

Mtandao wa Kitaifa wa CNG: Hali Ilivyo Sasa
Mradi wa Kisemvule-Mbagala haujitokezi kwenye ombwe; unakuja wakati ambapo taifa tayari limeanza kupiga hatua za dhati katika matumizi ya nishati ya CNG, ingawa bado kuna safari ndefu ya kwenda.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali ya Februari 2026, nchi nzima ilikuwa na jumla ya vituo kumi na moja (11) vya CNG, ambapo vituo tisa (9) vilikuwa jijini Dar es Salaam, kimoja mkoa wa Pwani na kingine mkoa wa Mtwara.
Idadi hiyo ndogo, ukilinganisha na mahitaji ya taifa, tayari imeambatana na mwamko mkubwa miongoni mwa wamiliki wa vyombo vya moto: takwimu iliyochapishwa mwezi huohuo zinaonyesha zaidi ya magari 15,000 nchini yalikuwa tayari yakitumia CNG, kutoka kwenye magari binafsi hadi bajaji, dalili tosha kuwa soko la nishati hii safi na nafuu linakua kwa kasi kuliko miundombinu iliyopo kuihudumia.
Serikali, kupitia TPDC, imekiri pengo hilo na inaonesha nia ya kulizibua kwa kasi zaidi.
Taarifa nyingine ya TPDC ya mwaka 2026 inaeleza mpango wa kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 22.06 katika ujenzi wa vituo vinavyohamishika (mobile CNG stations) katika mwaka wa fedha 2026/27, hatua itakayosaidia kusogeza huduma karibu zaidi na maeneo yasiyo na miundombinu ya kudumu ya mabomba.

Ni ndani ya muktadha huu wa kitaifa unaokua ndipo mradi wa bomba la Kisemvule-Mbagala, pamoja na mtandao wake wa vituo vitano vitakavyofuata, unapopata uzito wake wa kipekee, si tu kama uwekezaji mmoja wa kibinafsi, bali kama tofali muhimu litakalosaidia kuharakisha lengo pana la taifa la kuwa na mtandao imara, salama na wa uhakika wa nishati safi na nafuu kwa Watanzania wengi zaidi.
Kuelekea nishati safi ya kupikia
Mpango wa mbali zaidi wa mradi huu ni majumbani. Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia mwezi Mei 2024, ukiweka lengo la angalau asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Gesi asilia ya mabomba ni miongoni mwa suluhisho mojawapo linaloweza kufikia kaya nyingi za mjini kwa gharama ndogo ya matumizi ya kila siku.
Uwepo wa mfumo wa usambazaji kupitia Mbagala unaweka msingi mara njia kuu na mtandao wa ndani unapokuwepo, muunganiko wa kaya unakuwa karibu zaidi.
Rashal Energies imeeleza kuwa bomba limebuniwa likizingatia upanuzi huo wa baadaye.
Ni suala pia la afya ya jamii.
Uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba unaotokana na nishati za jadi za kupikia unahusishwa na vifo vya makumi ya maelfu nchini Tanzania kila mwaka, jambo ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi wanawake na watoto.
Kila kaya inayoachana na matumizi ya mkaa ni faida inayoweza kupimika.
Hata hivyo utekelezaji wa miundombinu ya CNG kwa ajili ya Kituo Kikuu cha Mbagala na vituo vidogo vya Vijibweni na DIT umekabidhiwa kwa muungano wa makampuni saba yenye utaalamu wa kipekee kuanzia ujenzi wa miundombinu, utengenezaji na ufungaji wa mabomba, mawasiliano ya simu, teknolojia ya ufuatiliaji wa kidijitali, hadi vifaa maalum vya CNG.
Muundo huu wa ushirikiano unalenga kupunguza hatari za ucheleweshaji, kuhakikisha ubora na uzingatiaji wa taratibu, na kuepusha changamoto za kiufundi wakati wa uzinduzi huku ukijumuisha matumizi makubwa ya bidhaa na huduma za ndani.
Mradi sasa umeingia awamu ya kuongeza kasi. Timu za ziada za ujenzi zinapelekwa ili kufungua maeneo kadhaa ya kazi kwa wakati mmoja, huku timu maalum zikipangwa kushughulikia sehemu mbili nyeti za hali ya hewa kwenye njia hiyo mto Mzinga na Bwawa la Vikundu ili zote zikamilike ndani ya Septemba, kabla ya mvua za El Niño zinazotarajiwa.
Kampuni inaeleza kuwa kasi hii inatokana na uhusiano mzuri wa kikazi uliojengwa kwenye ukanda huo. Wawakilishi wa TANROADS, TANESCO, DAWASA na TTCL wapo eneo la mradi na timu za mradi kila siku, huku mamlaka za Wilaya za Kisemvule na Mbagala zikisaidia upatikanaji wa maeneo na ushirikiano wa jamii katika kipindi chote.
Katika taarifa yake, Rashal Energies Limited ilisema mradi huu unafadhiliwa na Watanzania, kuhandisiwa na Watanzania na kujengwa na Watanzania, kwa manufaa ya viwanda na kaya za Kitanzania, ikisisitiza kuwa gesi ni mali ya taifa, na ujuzi wa kuisambaza unapaswa pia kuwa mali ya Watanzania. Gesi inayosafirishwa kwenye bomba hili inatolewa na TPDC.
Bomba la Gesi Asilia kutoka Kisemvule hadi Mbagala linaelezwa kuwa hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kijani, msingi imara wa viwanda, na jamii yenye uwezo zaidi.
TPDC inastahili kupongezwa kwa kuweka mazingira wezeshi yanayoamini uwezo wa ndani, lakini ni uwekezaji wa kijasiri, ustadi wa kiufundi, na uongozi thabiti wa Farhiya Warsame na Rashal Energies unaoleta dira hii nyumbani.
Huku timu zikijiandaa kushinda maeneo magumu ya Mto Mzinga na Bwawa la Vikundu kabla ya mvua za msimu, Watanzania wanaweza kusherehekea shujaa wa nishati wa ndani anayewaongoza kuelekea mustakabali safi na wa kujitegemea.


