Na Tatu Mohamed
CHUO cha VETA Dar es Salaam kinatarajia kuanza kutoa mafunzo maalumu ya urejelezaji taka (recycling) kuanzia Oktoba mwaka huu, yakilenga kuwajengea vijana ujuzi wa kutambua, kuchambua na kuchakata taka na kuzigeuza kuwa fursa za ajira na kipato.
Hatua hiyo imekuja baada ya chuo hicho kufanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kutekeleza mtaala wa mafunzo ya usimamizi wa taka na urejelezaji, ambapo VETA Dar es Salaam imechaguliwa kuwa moja ya vyuo vya majaribio (pilot) vya programu hiyo.
Akizungumza katika majadiliano hayo leo Septemba 8, 2026 Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, Abraham Mbughuni, amesema mafunzo hayo hayatalenga watu wanaojihusisha moja kwa moja na ukusanyaji na uchakataji wa taka pekee, bali pia jamii kwa ujumla kwa kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha taka.

Amesema elimu hiyo ni muhimu kwa kuwa itasaidia jamii kutambua thamani ya taka na namna zinavyoweza kutumika kama chanzo cha ajira na kipato.
“Wazalishaji wakubwa wa taka ni jamii kwa ujumla. Kwa hiyo mafunzo haya si kwa wale wanaochakata, kuchambua au kubeba taka pekee, bali ni muhimu pia kwa jamii inayozalisha taka,” amesema.
Amefafanua kuwa, VETA pia inalenga kuwapatia mafunzo wahusika wanaojishughulisha na kazi za taka ili waweze kufanya shughuli hizo kwa kuzingatia afya na usalama kazini, kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza katika kazi hiyo.

Amesema wahitimu watapatiwa vyeti na ujuzi unaohitajika ili kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi, huku akiwataka viongozi wa mitaa na kata kusaidia kutambua wananchi watakaonufaika na mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Jackline Wikechi, amesema mpango huo ni hatua muhimu katika kubadili mtazamo wa jamii kuhusu taka, ambazo mara nyingi zimekuwa zikionekana kama uchafu badala ya fursa.

Amesema NEMC haiwezi kukabiliana na changamoto ya taka peke yake, hivyo ushirikiano na taasisi za mafunzo kama VETA ni muhimu katika kuwajengea vijana ujuzi wa kuzitambua na kuzichakata taka.
“Naomba Watanzania waweze kuziona taka kama fursa, yaani ni kazi ambayo ni sawa na kazi nyingine, badala ya kuzidharau kwa sababu tu zinaitwa taka. Taka zinaweza kugeuka kuwa ajira ya kudumu, zikampa mtu heshima na kipato,” amesema Wikechi.
Amesema kupitia mtaala huo, vijana watafundishwa namna ya kutumia taka za aina mbalimbali kutengeneza bidhaa au fursa za kiuchumi, hatua ambayo inaweza kuongeza kipato na kuchangia katika ajira.
Naye Afisa Afya wa Kata ya Keko, Haji Hatibu Kikwacha, amesema anaunga mkono kuanzishwa kwa programu hiyo akieleza kuwa changamoto ya taka bado ni kubwa katika mitaa, hivyo elimu ya urejelezaji inaweza kusaidia kupunguza kiasi cha taka kinachobaki bila kutumika.

Amesema viongozi wa mitaa wako tayari kushirikiana katika kutoa elimu hiyo kwa wananchi kupitia mikutano ya wananchi inayofanyika katika maeneo yao.
“Swala la takataka ni changamoto katika mitaa yetu. Kwa hiyo tunahitaji jambo hili la recycling lifanyike kwa wakati na kwa ufasaha ili taka zinazoweza kurejelewa zitumike na kupunguza taka zinazobaki,” amesema.
Kikwacha amesema elimu hiyo itatolewa pia kupitia mikutano ya wananchi katika mitaa, ili kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kuchambua na kurejeleza taka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Magulumbasi A, Kata ya Keko, Hamis Nyanza, amesema elimu hiyo imemsaidia kubadili mtazamo kuhusu taka na kuahidi kushirikiana na VETA kuwahamasisha wananchi kushiriki katika mpango huo.

Amesema awali baadhi ya wananchi katika eneo lake walikuwa wakiziona taka kama uchafu pekee, lakini mafunzo hayo yameonesha kuwa zinaweza kuwa chanzo cha fursa na kipato.
“Kwa elimu ya leo kama kiongozi wa mtaa nimejifunza na ninaahidi kutoa ushirikiano mzuri kwa kuwahamasisha wananchi wangu waweze kupata elimu hiyo na kutambua kuwa taka zinaweza kuwa fursa,” amesema.
Programu hiyo inatarajiwa kuhusisha wadau mbalimbali wa mazingira, afya na serikali za mitaa ili kuhakikisha mafunzo yanawafikia vijana na wananchi wanaojihusisha na shughuli za ukusanyaji, uchambuzi na urejelezaji wa taka.


