📌 Nyumba za wafanyakazi zakarabatiwa, kuboresha utendaji wa kazi
📌 Mtambo wa kisasa wa kuchakata maji wazinduliwa
📍 MWANGA, KILIMANJARO | Septemba 2, 2026
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua na kukabidhi nyumba zilizokarabatiwa kwa wafanyakazi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa Maji cha Nyumba ya Mungu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Nyumba hizo, zilizojengwa tangu mwaka 1969, wakati Kituo cha Nyumba ya Mungu kilipoanza kufanya kazi, zimefanyiwa ukarabati mkubwa hatua inayolenga kuboresha mazingira ya makazi na ustawi wa wafanyakazi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi na makabidhiano hayo, Afisa Rasilimali Watu wa Kituo cha Nyumba ya Mungu, Bi. Neema Mwaisaka, amewataka wafanyakazi waliokabidhiwa nyumba hizo kuzitunza ili ziendelee kuwa na thamani na kutumika kwa muda mrefu.

“Natoa rai kwa wafanyakazi ambao tumewakabidhi nyumba hizi wazitunze, kwani Shirika limetumia fedha nyingi katika kuzikarabati,” amesema Bi. Neema.
Kwa upande wao, wafanyakazi waliokabidhiwa nyumba hizo, kupitia mwakilishi wao Masasi Maduka, wameipongeza Menejimenti ya TANESCO kwa kuboresha mazingira yao ya kuishi, wakieleza kuwa mazingira bora ya makazi yataongeza morali, ufanisi na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.

“Kuboresha mazingira yetu ya kuishi kutatuongezea morali ya kufanya kazi na kutuwezesha kujituma zaidi katika kutekeleza majukumu yetu,” amesema Masasi.
Katika hatua nyingine, Kituo cha Nyumba ya Mungu kimezindua mtambo wa kisasa wa kuchakata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu pamoja na matumizi katika mitambo ya kituo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtambo huo, Mkuu wa Kitengo wa Kituo cha Nyumba ya Mungu, Mha. Andrea Shio, amesema TANESCO imefanya ukarabati na uboreshaji wa mtambo huo ili kuufanya kuwa wa kisasa na kuongeza ufanisi wake.

“Naipongeza Menejimenti ya Shirika kwa ukarabati wa mtambo huu. Maji haya yanatumika kwa matumizi ya binadamu pamoja na kwenye mitambo,” amesema Mha. Shio.
Ukarabati wa nyumba za wafanyakazi pamoja na kuboresha miundombinu muhimu kama mtambo wa kuchakata maji ni sehemu ya jitihada za TANESCO za kuimarisha mazingira ya kazi na makazi, kuongeza ufanisi na kuhakikisha huduma za uzalishaji umeme zinaendelea kutolewa kwa uhakika.



